Habari za Kitaifa

HABARI ZA HIVI PUNDE: Yafichuka sasa kwamba habari za polisi za kupatikana kwa Muloki si kweli

Na KEVIN MUTAI, MERCY KOSKEI October 1st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

ZAIDI ya saa 10 tangu Idara ya Polisi kufichua kwamba dereva wa teksi Victoria Mumbua Muloki aliyekuwa ametoweka amepatikana akiwa amepoteza fahamu Migori, familia yake bado haijajulishwa kuhusu aliko.

Jumatatu jioni, mamake Victoria, Anne Kanini alikuwa ameambia Taifa Leo kwamba walipokea habari kwamba amepatikana na kwamba kulikuwa na mipango ya kumsafirisha kwa ndege hadi Mombasa.

Taifa Leo ikamtafuta kwa simu Msemaji wa Polisi Resila Onyango ambaye alithibitisha habari hizo mwendo wa saa moja jioni.

Dkt Onyango alithibitisha kwamba Bi Muloki alipatikana akiwa hali mahututi karibu na bwawa la Uriri, Kaunti ya Migori.

“Tulimpata akiwa amepoteza fahamu karibu na kingo za Bwawa Uriri, akiwa na majeraha mabaya ya mikono na kichwani,” alisema.

Aliongeza kusema kwamba Muloki alipelekwa katika kituo cha afya kilicho karibu kwa matibabu na kwamba familia yake ilikuwa imeshajulishwa kuhusu hilo.

Hata hivyo, kufikia saa tisa alasiri Jumanne, Oktoba 1, 2024, familia na vyombo vya habari hawakuwa wamepata habari zozote zaidi kuhusu aliko Muloki. Hii ni licha ya Taifa Leo kuweka juhudi za kupata habari kutoka kwa polisi.

Sasa imebainika kwamba makao makuu ya Idara ya Polisi na familia ya Bi Muloki mjini Mombasa huenda walihadaiwa na watu wasiojulikana.

Mamake aliambia Taifa Leo kwamba walituma Sh20,000 kwa mtu fulani mjini Migori aliyewaambia kwamba pesa hizo zingesaidia kumsafirisha kwa ndege hadi Mombasa.

Bi Kanini alisema bado hawajafahamishwa kuhusu aliko binti yao kufikia Jumanne alasiri.

“Napanga kwenda kwenye makao makuu ya polisi ili niambiwe kinachoendelea,” Bi Kanini akasema kwa njia ya simu.

Akizungumza Jumanne nje ya mahakama mjini Nakuru, mpwa wa Mumbua Mbithe Muigai alieleza kushangazwa na ripoti za polisi zilizodai kwamba shangazi yake amesafirishwa kwa ndege kwenda Mombasa kwa matibabu.

Alithibitisha kwamba kufikia Jumatatu jioni, mtu fulani alimpigia simu pasta wa shangazi yake mjini Mombasa, akidai kuwa afisa wa polisi kutoka Migori, na akataka atumiwe Sh20,000.

Mpigaji simu huyo alidai kwamba Muloki alipatikana akiwa amepoteza fahamu na pesa hizo zilihitajika kumsafirisha kwa matibabu ya dharura.

Baada ya kupokea pesa, mwenye simu hiyo aliizima na kuzua sintofahamu huku ripoti zikidai polisi wamempata Muloki akiwa hai.

“Hatujampata, na hatuna habari zozote kuhusu aliko,” akasema Bi Muigai.