Habari za Kitaifa

Hakimu aachilia huru mvulana, 15, aliyeshtakiwa kunajisi msichana wa umri wa miaka 18

Na TITUS OMINDE December 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MWANAFUNZI wa Darasa la Saba mwenye umri wa miaka 15 katika shule moja ya msingi jijini Elodret atakumbuka jinsi alivyozuiliwa katika rumande ya watoto kwa miezi minne kwa madai ya kunajisi msichana anayekaribia kutimiza umri wa miaka 18.

B.K alilazimika kuacha masomo yake kwa muda wa miezi minne kwa kuwa alikuwa kizuizini akisubiri uchunguzi wa tuhuma za unajisi.

Kesi yake ilivutia mawakili wawili wakuu kutoka Eldoret ambao walijitolea kumpa huduma za uwakilishi wa bure walipogundua kuwa mvulana huyo alikuwa mwathiriwa wa sheria ya kingono yenye utata ya 2006.

Kutokana na kesi hiyo, mawakili Nathan Oburu na Samuel Ondieki wamefufua mjadala mkali wa kutaka sheria hiyo ifanyiwe marekebisho au la, haswa kwa kupunguzwa kwa umri wa idhini ya kujamiiana kutoka 18 hadi 16.

Huku akipinga kuzuiliwa zaidi kwa mtoto huyo, wakili Oburu alitetea mteja wake kwa kusema kuwa msichana huyo ndiye aliyepswa kushtakiwa kwa kumnajisi mvulana husika.

“Mshukiwa katika kesi hii ni mdogo zaidi kuliko mlalamishi, ikiwa kuna lolote msichana huyo ndiye aliyepaswa kushtakiwa kwa kumnajisi mteja wangu,” Bw Oburu aliambia Hakimu Mkuu wa Eldoret Peter Areri.

Msimamo sawa ulishikiliwa na wakili mwenzake maoni yake yakiungwa mkono na mwenzake Samuel Ondieki aliyeiomba mahakama kumwachilia mtoto huyo bila masharti yoyote.

“Kwa kuzingatia kwamba mvulana aliye mbele yako ana umri wa miaka 16 tu wakati mlalamishi anakaribia miaka 18. Mahakama inafaa kumwachilia mvulana huyu baada ya kuteseka rumande kwa zaidi ya miezi minne,” akasema Bw Ondieki.

Akitoa uamuzi wake, hakimu Areri alisema kuwa kukamatwa na kuzuiliwa kwa mvulana huyo ni kinyume cha sheria.

“Kukamatwa na kuzuiliwa kwa mshukiwa hakukuwa halali. Uko huru nenda nyumbani,” aliamuru Bw Areri.