Habari za Kitaifa

Hakimu aagiza DCI kukamata makarani wa korti kwa kumpaka tope

Na RICHARD MUNGUTI April 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KATIKA kisa cha kushtua na kubainisha ukweli, hakimu wa mahakama ya Kilgoris anayedaiwa alipokea hongo ya Sh2 milioni ameamuru maafisa wa uchunguzi wa jinai (DCI) wawakamate makarani wa hiyo korti kuandikisha taarifa kuhusu madai hayo.

Na wakati huo huo Bw Cyprian Waswa Wafula aliwaamuru maafisa DCI wawatie nguvuni mshukiwa na mlalamishi katika kesi ya kutisha kuua kuandikisha taarifa na kuwahoji na kuwachunguza kuhusu madai hayo.

Agizo hili linafuatia ufichuzi wa Bw Waswa mahakamani kwamba amedaiwa katika mitandao ya kijamii kwamba amekula hongo ya Sh2 milioni kutweza haki katika kesi inayowakabili Olondarai Tasur almaarufu Saningo na Samuel Sankei Tasur.

Olondarai na Sankei wanakabiliwa na shtaka la kutisha kumuua Daniel Lesham Seitai.

Olondarai na Sankei walishtakiwa walitisha kumuua Lesham kwa mishale mnamo Machi 24, 2025 katika eneo la Kilenaira, Transmara Magharibi, Narok.

“Kabla ya kesi hii kuanza nataka Olondarai na Sankei waeleze mahakama kuhusu madai nilipokea hongo ya Sh2 milioni kutweza haki,” Bw Waswa alisema Jumanne, Aprili 1, 2025.

Hakimu huyo pia aliwataka makarani wa mahakama hiyo ya Kilgoris kueleza kinaga ubaga ikiwa walipokea Sh2 milioni kutoka kwa ukoo wa washtakiwa ama mlalamishi kwa niaba yake.

“Hili jambo sio rahisi vile mnaichukulia. Nimepokea simu kutoka Ikulu ya Nairobi kuhusu kesi hii,” alisema Bw Waswa.

Hakimu huyo alisema ikiwa washtakiwa walichangiwa pesa kumhonga kutoka kwa ukoo wao waeleze adharani.

“Madai kwamba nimepokea pesa za hongo zimeenea kote katika mitandao ya kijamii na hata jarida moja la kila wiki limezichapisha,” alisema Bw Waswa.

Hakimu alisema madai hayo yamemharibia sifa na lazima mwenye kuyaeneza achukuliwe hatua kali kisheria.

Bw Waswa alisema hawezi kuanza kujibizana na watu mitandaoni lakini, lazima walioeneza madai hayo wawajibike.

“Madai haya yamenichafulia jina pamoja na idara ya mahakama kwamba inapokea hongo kutotenda haki,” alisema Bw Waswa.

Mawakili Danstan Omari na Stanley Kinyanjui waliomba hakimu achukue hatua kali kwa wanaoeneza uvumi na madai hayo.

“Hakuna hakimu ama jaji anayeweza kufanya kazi kwa vitisho. Lazima walioneza uvumi huu wachukuliwe hatua kali,” alisema Bw Omari aliyeomba hakimu ajiondoe kwenye kesi hiyo.

Bw Waswa alijiondoa kwenye kesi hiyo na kuamuru maafisa wa DCI wawatie nguvuni makarani na washukiwa, pamoja na mlalamishi kuhojiwa kuhusu madai hayo ya upokeaji rushwa.

“Naamuru makarani wa hii mahakama wakamatwe kuandikisha taarifa kuhusu madai hayo ya ulaji rushwa ya Sh2 milioni. Ikiwa ni wao walipokea kitita hicho wakidai ni cha hakimu basi wabebe mzigo wao,” Bw Waswa aliagiza.

Pia, aliagiza washtakiwa wote wawili na mlalamishi wakamatwe na kuhojiwa.

Hakimiu alifichua kwamba tayari ameandikisha taarifa kwa maafisa wa DCI.