Habari za Kitaifa

Hakuna tofauti yoyote kati ya falsafa za UDA na ODM – Mbadi 

Na LABAAN SHABAAN August 3rd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

WAZIRI mteule wa Hazina ya Kitaifa, John Mbadi, amekiri kuwa chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) na kile cha upinzani Orange Democratic Movement (ODM) havina tofauti kifalsafa.

Bw Mbadi alisema haya Jumamosi alipokuwa akihojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi katika Bunge la Kitaifa baada ya kuteuliwa Waziri wa Fedha.

“Falsafa za vyama vya UDA na ODM hazina tofauti sababu zinaangazia demokrasia ya kijamii. Vyama hivi vinashughulikia ajira, gharama ya maisha, kilimo na uchumi wa majini,” alisema Bw Mbadi akijibu swali la mwanakamati Junet Mohamed, Mbunge wa Suna Mashariki.

Alifunguka kuwa alitarajiwa kuulizwa swali hili lakini hakutarajia litoke kwa mbunge wa upande wa Upinzani (ODM).

“Nilijua swali hili litaulizwa lakini si na Junet,” alikiri na kuzua kicheko ukumbini.

Kabka ya kuteuliwa kwake, Bw Mbadi alikuwa mkosoaji mkali wa Serikali ya Kenya Kwanza hasa kuhusu jinsi ilivyokuwa ikishughulikia suala la msukosuko wa uchumi nchini.