Habari za Kitaifa

Hatuko kwenye mashindano, Ruto aambia makanisa akijibu ukosoaji wa makasisi

Na CHARLES WASONGA December 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amekariri kuwa kanisa na serikali sharti zifanye pamoja kwa manufaa ya wananchi wa Kenya, akisema hazifai kuvutana.

Kiongozi wa taifa pia aliwataka viongozi wa kisiasa kutoka mirengo mbalimbali kukomesha malumbano ya kila mara huku akiahidi kuwa serikali yake itahudumia raia wote bila ubaguzi.

Akiongea Jumapili wakati wa ibada maalum iliyoshirikisha viongozi wa makanisa mbalimbali katika eneo la Kimana, eneo bunge la Kajiado Kusini, Dkt Ruto alisema kuwa Kenya haitastawi katika mazingira ya mivutano, haswa inayolenga kuwagawanya wananchi.

“Hamna mashindano kati ya kanisa na wengine, au kati ya kanisa na serikali. Ningependa kusisitiza hapa kwamba hakuna haja ya kuwepo kwa mvutano kati ya Kanisa na Serikali kwa sababu sote tunawahudumia raia,” Dkt Ruto akasema.

‘Manufaa ya taifa’

“Sharti tuungane; sharti tufanye kazi pamoja. Kanisa na Serikal sharti zifanye kazi pamoja, viongozi kutoka jamii zote sharti wafanye kazi pamoja na viongozi kutoka vyama mbalimbali vya kisiasa sharti wafanye kazi kwa manufaa ya taifa hili. Hatutaki chuki na mashindano yalisiyo na maana wala manufaa kwa watu wetu,” Rais Ruto akaongeza.

Katika siku za hivi karibuni viongozi mbalimbali wa makanisa wameikosoa serikali ya Rais Ruto kwa utawala mbaya unaovumilia ufisadi na vitendo vya ukiukaji wa haki za kibinadamu kama vile utekaji nyara wa watu wanaosawiriwa kuwa wakosoaji wa serikali.

Viongozi wa Kanisa Katoliki, Kanisa la Kianglikana (ACK) na Makanisa na Kipentekosti na Kivanjelisti pia wameikosoa serikali ya Rais Ruto kwa kuendeleza sera kandamizi kwa raia wa kawaida kwa kuwaongezea gharama ya maisha.

Rais Ruto na wandani wake pia wamekosolewa kutokana na mtindo wao wa kutoa mamilioni ya fedha kama “sadaka” kanisani, viongozi wa kidini wakishuku kuwa hizo ni pesa zilizopatikana kwa njia ya ufisadi.

Majuma mawili yaliyopita, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki jimbo la Nairobi Philip Anyolo aliamuru kurejeshwa kwa Sh2.6 milioni ambazo Rais Ruto alitoa katika Kanisa Katoliki la Soweto Nairobi.

Hata hivyo, akiongea katika ibada ya Jumapili wiki jana katika eneo la Kipsitet, eneo bunge la Sigowet/Soin, Kaunti ya Kericho, Rais Ruto alisema kuwa ataendelea kusaidia mipango na miradi ya Kanisa kwa sababu amekuwa akifanya hivyo kwa miaka 30 iliyopita.

Wasiogope kuitisha usaidizi

Jumapili, Rais Ruto alirudia kauli hiyo akiwaambia viongozi wa Kanisa katika Kaunti ya Kajiado wasiogope kuitisha usaidizi kutoka kwake kwani “mimi ni mwinjilisti na ninataka neno la Mungu lihubiriwe kote.”

“Msijali kuwa wale wamerudisha mchango wangu. Nitawapa yenu.” Rais Ruto akasema bila kutaja kiasi halisi cha pesa ambazo anapania kutoa kwa makanisa hayo.

Kiongozi wa taifa pia alikariri kujitolea kwake kutimiza ahadi zote ambazo alitoa kwa Wakenya kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022.

“Na katika kufanya hivyo, ninaahidi kuwa sitabagua kwa misingi ya dini, kabila, eneo au watu wa imani fulani. Maendeleo ya serikali yatawafikia watu wote kwa usawa,” akasema.

Rais Ruto aliahidi kuwa serikali yake itazindua Februari mwaka ujao mradi wa kuweka lami barabara ya Illasit-Rombo-Taveta, ili kuwawezesha wakulima wa Kajiado Kusini kufikisha mazao ya shambani sokoni.

Aidha, aliahidi kuwa serikali yake imetenga pesa za kufadhili ujenzi wa masoko katika eneo la Kimana, Rombo na Isinet.