Habari za Kitaifa

Historia Olimpiki: Nani kama Faith Kipyegon!

Na GEOFFREY ANENE August 10th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NYOTA Faith Kipyegon amethibitisha hana kifani katika mbio za mita 1,500 duniani baada ya kuandikisha historia ya kuwa wa kwanza kabisa kuzoa dhahabu tatu mfululizo za Olimpiki, jijini Paris, Ufaransa, Jumamosi usiku.

Kipyegon alionyesha ujasiri mkubwa kufyatuka kama mshale alipopiga kona ya mwisho na kutwaa taji kwa rekodi mpya ya Olimpiki ya dakika 3:51.29.

Kipyegon, 30, alishikilia rekodi ya awali ya Olimpiki aliponyakua taji lake la pili katika mbio hizo za kuzunguka uwanja mara nne; dakika 3:53.11 jijini Tokoyo, Japan, mwaka 2021.

Kipyegon akimaliza wa kwanza na kushinda dhahabu mbio hizo za 1,500m jijini Paris. PICHA | REUTERS

Katika fainali hiyo ya Jumamosi malkia huyo alifuatwa kwa karibu na Jessica Hull kutoka Australia (3:52.56) na Muingereza Georgia Bell (3:52.61), huku mbinu za Ethiopia kuchoma watimkaji kwa kasi ya juu katika mizunguko mitatu ya kwanza zikisambaratika katika mita 200 za mwisho.

Kipyegon alishikilia rekodi ya mataji mawili ya Olimpiki ya 1,500m kwa pamoja na mshindi wa 1976 na 1980 Tatyana Kazankina kutoka Urusi na rais wa Shirikisho la Riadha Duniani Sebastian Coe (1980 na 1984), lakini sasa anashikilia rekodi hiyo pekee yake baada ya kuzoa taji la tatu mfululizo Jumamosi.

Mkenya mwingine aliyefika fainali ya 1,500m, Susan Ejore, alikamata nafasi ya sita kwa 3:56.07 katika makala hayo ya 33 jijini Paris.

Kwemoi amaliza ukame wa 5,000m

Kipyegon aliweka historia dakika chache tu baada ya Rodgers Kwemoi kushindia Kenya medali ya 5,000 ya wanaume kwa mara ya kwanza kabisa katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

Medali ya Kwemoi ilishangiliwa kwa furaha tele kwani Kenya ilitoka mikono mitupu katika 5,000m za wanaume kwenye Olimpiki za Rio 2016 na Tokyo 2020.

Wakenya wengine waliowahi kushinda medali katika mbio hizo za kuzunguka uwanjani mara 12 na nusu ni John Ngugi (dhahabu mwaka 1988 mjini Seoul), na washindi wa fedha Kipchoge Keino (1968 mjini Mexico City), Paul Bitok (1992 mjini Barcelona na 1996 mjini Atlanta) na Eliud Kipchoge (2008 mjini Beijing).

Ronald Kwemoi (kushoto) baada ya kushinda fedha katika 5,000m huku Edwin Kurgat akimpongeza jijini Paris, Jumamosi usiku. PICHA | REUTERS

Naftali Temu alinyakualia Kenya medali yake ya kwanza kabisa katika 5,000m kwenye Olimpiki mwaka 1968 (shaba). Eliud Kipchoge pia aliambulia shaba mwaka 2004 mjini Athens nchini Ugiriki, sawa na Edwin Soi (2008 Beijing) na Thomas Longosiwa (2012 London).

Kufuatia ushindi wa dhahabu wa Kipyegon (1,500m), Emmanuel Wanyonyi (800m) na fedha kutoka kwa Kwemoi (5,000m), Kenya ilipanda nafasi 10 kwenye jedwali la medali na kutulia nambari 16 kati ya timu 205 zinazoshiriki mashindano hayo mjini 205.

Bingwa wa Jumuiya ya Madola 5,000m Beatrice Chebet alizoa dhahabu ya 5,000m na 10,000m. Malkia mara tatu wa dunia 1,500m Kipyegon alinyakua fedha ya 5,000m nao Mary Moraa (800m), Faith Cherotich na Abraham Kibiwot (3,000m kuruka viunzi na maji) na Benson Kipruto (marathon) wakapata shaba.