Hofu Rais Ruto anapigana vita vingi mno
RAIS William Ruto anaonekana kuanzisha mapambano makali katika kila pembe na huenda yakayumbisha utendakazi wa serikali ya Kenya Kwanza.
Kiongozi wa nchi kwa sasa anakabiliwa na shinikizo za kutupa Mswada wa Fedha 2024 ambao ulipita bungeni wakati wa kusomwa kwa mara ya pili wiki jana.
Leo kutakuwa na maandamano makubwa nchini kupingwa mswada huo wabunge wakitarajiwa kuupigia kura tena.
Makanisa na viongozi wa upinzani ni kati ya wale ambao wameungana na vijana kupinga mswada huo. Makundi hayo yote yamekuwa yakisisitiza kuwa masuala ambayo yanaibuliwa na vijana lazima yatatuliwe.
Viongozi wa upinzani nao wanaendeleza shinikizo wakitaka mswada huo utupiliwe mbali wote kutokana na mapendekezo ya ushuru wanayoyasema yanawaumiza raia.
Ndani ya serikali, hali si hali kwa Rais huku akitofautiana na Naibu Rais Rigathi Gachagua kutokana na masuala mbalimbali ya uongozi.
Wachanganuzi wa kisiasa sasa wanasema kuanzisha vita kila kona na wanasiasa pamoja na kizazi cha sasa kutalemaza na kuyumbisha serikali ya Kenya Kwanza.
Madai ya Bw Gachagua kuwa kuna baadhi ya wanasiasa ambao wanatumia urafiki wao na Rais kumwaamrisha yalianika jinsi uhusiano kati ya viongozi hao wakuu unavyoendelea kudorora.
Pia Bw Gachagua amewashutumu baadhi ya wanasiasa kutoka Ukanda wa Mlima Kenya ambao ni wandani wa rais, akisema wanatumiwa kumpiga vita kisiasa.
Ingawa hivyo, maandamano yanayoendelea ya vijana kuhusu mswada wa fedha, ndiyo yanaonekana yametikisa serikali zaidi. Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi tayari anahofia hali, akisema kuwa mswada huo kuanguka ni kama kupigwa kura ya kutokuwa na imani na Rais Ruto.
Bw Mudavadi alidai kuwa wale ambao wanakataa Mswada wa Fedha 2024, wanapanga njama ya kumwondoa Rais Ruto afisini.
“Mswada ukikataliwa, kile ambacho kitafuata ni kura ya kuondoa serikali mamlakani ili uchaguzi mpya uandaliwe,” akasema Bw Mudavadi, kauli ambayo ilionyesha wazi jinsi ambavyo serikali imetiwa uoga na maandamano hayo.
Wandani wa Rais wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah nao wamewapuuza vijana wanaoandamana akisema wengi wao wanatoka familia zenye uwezo na hawafahamu serikali inavyopanga kugatua huduma mashinani.
Kwa mujibu wa mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Oloo, serikali lazima ijitokeze na kuwasikiza vijana na njia pekee ni kuachana na Mswada wa Fedha 2024.
“Serikali inataka kuwatoza ushuru hata Wakenya ambao hawana kazi. Hii ndiyo maana vijana wamezinduka na sasa wanaandamana kwa sababu hawana kazi na wanalimbikiziwa ushuru,” akasema Bw Oloo kwenye mahojiano na Taifa Leo.
Kando na ushuru, Rais Ruto pia anakabiliwa na uhasama wa kisiasa kati yake na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta ambaye afisi yake imelalamika kuwa haijakuwa ikipata mgao iliyotengewa.