Hofu visa vya kolera vikipanda nchini
VISA vya maradhi ya Kipindupindu vimeongezeka kutoka 69 hadi 97 huku watu sita wakifariki, Wizara ya Afya imeeleza.
Wizara ya Afya ilisema mapema wiki jana kupitia kwa taarifa kuwa kaunti za Kisumu, Nairobi na Migori zimeshuhudia vifo baada ya watu kadha kuathirika na maradhi hayo.
Kwa visa 32 vilivyoripotiwa Kisumu, watu wanne walifariki huku Migori ikiwa na visa 53 na mtu mmoja akipoteza maisha yake.
Katika kaunti ya Nairobi, visa 12 viliripotiwa na mtu mmoja akaaga dunia.
Kolera ni ugonjwa unaosababishwa na kula chakula au kunywa maji yaliyoathiriwa na bakteria.
Shirika la Afya Duniani (WHO), linasema kuwa mgonjwa huonyesha dalili za ugonjwa huu saa 12 hadi siku tano baada ya maambukizi.
Wakenya wameshauriwa kunywa maji safi badala ya kunywa au kupikia maji ya mto, ziwa na kuhakikisha kuwa wanahifadhi maji kwa chupa safi zilizo na vifuniko.
Pia, wameshauriwa kutotupa taka ovyoovyo na kutoenda haja kubwa na ndogo kiholela haswa karibu na maeneo ya maji.