Hofu ya Nyakang’o kuhusu deni la nchi
MDHIBITI wa Bajeti, Margaret Nyakang’o, ameelezea wasiwasi kuhusu uwazi wa baadhi ya mawasilisho ya serikali ya kitaifa kuhusu fedha za kulipa madeni inayokopa mashirika ya kifedha ya humu nchini, akisema hayana maelezo ya kina.
Dkt Nyakang’o alieleza Bunge la Kitaifa kuhusu Fedha kuwa tangu Julai mwaka uliopita, amepokea mawasilisho na malipo ya deni la kitaifa yaliyotekelezwa nje ya mfumo wa kielektroniki na kuzua wasiwasi kuhusu uwajibikaji na uwazi.
Akifichua yanayoendelea, Dkt Nyakang’o alisema afisi yake imeshindwa kufuatilia malipo na mawasilisho yanayofanywa kwa njia isiyo ya kielektroniki kwa sababu malipo kama hayo hayana nakala zinazoweza kukaguliwa.
Alipofika mbele ya kamati inayoongozwa na Mbunge wa Molo, Kimani Kuria kuhusiana na Taarifa ya Sera ya Bajeti (BPS), Dkt Nyakang’o alihoji sababu ya serikali kuamua kutekeleza baadhi ya malipo kupitia mfumo usiofaa ilhali kuna mfumo wa kielektroniki kwa shughuli hizo.
Mdhibiti huyo wa bajeti alieleza kundihilo kuwa malipo yaliyowasilishwa kwake kuidhinisha hayana maelezo ya kina kwa sababu huletwa yakiwa yamerundikana na kufanya iwe vigumu kwa afisi yake kubaini jinsi fedha hizo zinavyotumika kwa sababu malipo hufanywa nje ya mfumo rasmi.
“Ni sharti niwasilishe suala hili kupitia maandishi kwa Hazina Kuu kwa sababu sasa nina data ya kutosha. Mbona tunaendelea kufanya malipo kupitia mtindo wa zamani ilhali tuna mfumo wa kielektroniki,” alihoji Dkt Nyakang’o.
“Baada ya miezi mitatu, wanawasilisha mrundikano usioambatana na maelezo ya jinsi fedha zilitumika. Imetulazimu kukataa baadhi kwa kukosa maelezo ya kina,” alisema.
Japo Dkt Nyakang’o hakutaja kiasi cha fedha zilizolipwa na serikali tangu Julai mwaka jana, alihakikishia kamati kwamba, ana maelezo yote ya mawasilisho na atayakusanya ili yatumwe Bungeni Jumanne.
Alisema huwa anashughulikia faili 115 za mawasilisho kila wiki kuhusu malipo ya deni la umma na faili 30,000 kwa mwaka kuhusu malipo ya uzeeni.Alifichua kwamba, Januari mwaka huu, serikali ililipa Sh19.6 bilioni kupitia dola ya Amerika kwa benki za humu nchini zilizodhamini mkopo wa shirika la ndege la Kenya Airways.
Alihoji sababu ya benki za humu kuitisha malipo kupitia dola.Isitoshe, Dkt Nyakang’o alieleza kamati hiyo kuwa afisi yake ilipopokea ripoti ya serikali kuhusu matumizi ya Sh18 bilioni, kiasi hicho hakikuelezwa wazi.“Mambo haya hutokea. Wakati mwingine tunajaribu kupata maelezo lakini si rahisi,” alisema Dkt Nyakang’o.
Ili kusuluhisha masula hayo, Dkt Nyakang’o alifichua Benki Kuu ya Kenya (CBK) imeanzisha mfumo kwa jina ‘pacha” kuhakikisha kiasi cha fedha anachoidhinisha kinalingana na kinachotolewa na benki.
“Natumai mfumo huu mpya utafaulu,” alisema Dkt Nyakang’o.Mwenyekiti wa Kamati alimwagiza Dkt Nyakang’o kuwasilisha maelezo yote kuhusu mawasilisho yaliyotolewa kwa njia isiyo ya kielekitroniki katika bajeti ya mwaka huu.