Hofu ya Raila kubebeshwa maovu ya Ruto baada ya ‘handisheki’
ALIYEKUWA Waziri Mkuu Raila Odinga huenda akalaumiwa, pamoja na Rais William Ruto, na wakosoaji wa serikali kutokana na mapungufu ya zamani na yajayo, baada ya wawili hao kutia saini mkataba wa ushirikiano Ijumaa, Machi 7, 2025, wadadisi wameonya.
Ingawa Bw Odinga alifafanua kuwa mkataba huo hautoi nafasi ya kuundwa kwa muungano wa kisiasa katika ya vyama vya (United Democratic Alliance – UDA na Orange Democratic Movement – ODM), wandani wake watano wanahudumu kama mawaziri katika serikali ya Dkt Ruto.
Watano hao ambao ni; John Mbadi (Fedha), Wycliffe Oparanya (Vyama vya Ushirika), Ali Hassan Joho (Madini na Uchumi wa Majini), Opiyo Wandayi (Kawi) na Beatrice Askul Moe (Masuala ya Afrika Mashariki) waliteuliwa Julai mwaka jana, 2024, kufuatia maasi ya vijana wa Gen Z na wanatekeleza sera za serikali ya Dkt Ruto.
Aidha, kwenye hotuba yake baada ya kutia saini mkataba huo katika ukumbi wa KICC, Nairobi, Bw Odinga alisema “mkataba huo unaweza kuweka msingi wa ushirikiano kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027”.
“Ufanisi katika utekelezaji wa mkataba tuliotia saini leo unaweza kuweka msingi wa kuundwa kwa muungano mpana utakaoleta utulivu nchini,” Bw Odinga akaeleza.
Tayari kiongozi huyo wa ODM amelaumiwa na viongozi wa upinzani Kalonzo Musyoka na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa, wakidai hatua yake ya kushirikiana na Rais Ruto ni usaliti wa wananchi na haswa vijana wa taifa hili.
Bw Odinga alikabiliwa na lawama sawa na hiyo alipofanya handisheki na rais mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018.
Baada ya hapo, Bw Kenyatta alimuunga mkono kwa urais mnamo 2022 ambapo alishindwa na Dkt Ruto kwani “alibebeshwa mzigo wa utawala wa serikali.”
Japo hakujiuzulu wadhifa wake wa Naibu Rais, Dkt Ruto alionekana kutengwa serikalini baada ya Bw Kenyatta kutangaza alikuwa akiendesha serikali kutokana na ushauri kutoka kwa Bw Odinga “baada ya naibu wangu kutelekeza majukumu yake,”
Sasa kwa mara nyingine, Bw Odinga amejipata katika hali, aliyojipata kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022, ambapo huenda akaelekezewa maovu ya serikali.
Wakati za ziara zake sehemu mbalimbali nchini “kufanya mashauriano” na wafuasi wake kuhusu mwelekeo wa kisiasa ambao anapaswa kuuchukua, Bw Odinga alitaja masuala kadhaa ambayo hayaendi vizuri serikalini.
Alitaja utendakazi wa Mamlaka ya Afya ya Kijamii (SHA) inayosimamia bima mpya ya afya ya kijamii (SHIF), ushuru wa nyumba, ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, mgao mdogo wa fedha kwa serikali za kaunti, ugavi wa sawa wa miradi ya maendeleo na ujenzi wa masoko mapya kote nchini.
Lakini sasa Seneta wa Kisii, Richard Onyonka anaelezea hofu kuwa kiongozi wa chama chake cha ODM amebebeshwa mizigo anayofia inaweza kuharibu sifa zake.
“Ni vizuri kulazimisha serikali itekeleze majukumu yake ukiwa nje. Lakini kile Bw Odinga anafanya ni kurudia kosa ambalo alifanya na Uhuru 2018,” akasema Bw Onyonka.
Hata hivyo, Seneta Onyonka aliongeza kuwa kuna uzuri wa kuwa “ndani ya kwa sababu utajua jinsi adui wako anaendesha shughuli zake ili uweze kujua namna ya kumkabili siku zijazo,”.
Bw Onyonka akasema: “Njia ya kipekee kwa Raila ni kurekebisha maovu ya Ruto. Ndio njia ya kipekee itakayomwezesha kupata uungwaji mkono kutoka kwa raia.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nairobi Winnie Mitullah anasema nia ya Rais katika kutia saini mkataba na Bw Odinga ni kujifaidi kisiasa.