Hutaweza kutumia simu ambayo haijalipiwa ushuru, Serikali yatangaza
SERIKALI itaanza kufuatilia simu zote za mkononi zilizoagizwa kutoka nje au zilizotengenezwa nchini kuhakikisha kuwa watengenezaji na wasambazaji simu hizo wanalipa ushuru.
Hatua hii, itakayoanza kutekelezwa Januari mwaka ujao, ni sehemu ya mikakati ya serikali ya kupanua mawanda yake ya ukusanyaji ushuru.
Serikali imeagiza kuwa sharti kampuni zote za kutengeneza simu ziweke nambari za utambulisho za simu hizo (IMEI) kwa mtandao wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru (KRA).
“Hii itahakikisha kuwa simu zote zinalipiwa ushuru,” Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA) inasema.
Wakati huo huo, watu wote wanaonunua simu kutoka ng’ambo ili kuuza nchini watahitajika kufichua nambari za IMEI katika stakabadhi zao za uagizaji bidhaa kwa KRA.
Serikali inashikilia kuwa ni lazima simu zote za mkononi zisajiliwe katika Hifadhi ya Kitaifa ya Data kuhusu Mitambo iliyolipiwa Ushuru.
“Ili kudumisha uadilifu na ulipaji ushuru kwa simu zote za mkononi nchini, mamlaka hii inawajulisha wadau wote, zikiwemo kampuni za simu za mkononi, wanaojihusisha katika utengenezaji, uagizaji, usambazaji pamoja na uunganishaji wa simu hizo na mtandao ya humu nchini, kwamba kuanzia Januari 1, 2025 hitaji hili litaanza kutekelezwa,” tume ya CA ikasema kupitia tangazo kwa umma.
Kwa wauzaji na wa rejareja na wale wa jumla wa simu za mkononi, serikali imeamuru, kwamba sharti wahakikishe wanauza simu ambazo zilizolipiwa ushuru pekee.
Mamlaka ya CA itatangaza namna ambavyo wananunuzi na watumiaji simu hizo watathibitisha kuwa zimelipiwa ushuru.
Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo David Mugonyi anasema kampuni za kutoa mawimbi ya mawasiliano ya simu za mkononi kuhakikisha zinatoa huduma hiyo baada ya kuthibitisha kuwa simu husika zimelipiwa ushuru.
“Kampuni hizo pia zitahitajika kutoa orodha ya simu zisizolipiwa ushuru ili kufanikisha mpango wa kuhakikisha zinalipiwa ushuru, la sivyo simu hizo zitazimwa,” Bw Mugonyi akasema.
“Masharti hayo mapya yatatumiwa kwa simu zilitengenezwa au kuingizwa nchini kuanzia Novemba 1, 2024. Simu zote ambazo zimekuwa zikitumika kufikia Oktoba 31, 2024 hazitaathirika na masharti hayo,” CA ikaeleza.
Mamlaka ya CA ni asasi ya serikali inayosimamia sekta ya habari na mawasiliano (ICT) nchini. Sekta hiyo inashirikisha kampuni za mawasiliano, biashara za mitandaoni, usalama mitandano, utangazaji na huduma za posta.
Mamlaka hiyo pia husimamia utoaji wa masafa kwa mashirika ya utangazaji.CA pia inayo wa kufanikisha biashara katika sekta ya ICT na utoaji leseni kwa vifaa vinavyotumika katika biashara hiyo kupitia Shirika la Kenya Trade Network Agency (Ken Trade).