Idah Odinga apendekeza John Mbadi kumrithi Raila
NA JUSTUS OCHIENG
MKEWE kiongozi wa Azimio la Umoja, Bw Raila Odinga, Bi Idah Odinga amemwidhinisha Mbunge Maalum John Mbadi kuwa mrithi wa kisiasa wa mumewe.
Akihutubu Ijumaa, Februari 23, 2024 katika Kaunti ya Homa Bay, Bi Odinga alisema kuwa chama cha ODM kina “watu wengi wenye uwezo wa kukiongoza, hata ikiwa Bw Odinga hatakuwepo”.
Kauli yake inatokea huku mdahalo ukivuma kuhusu ni nani anayefaa kumrithi Bw Odinga kisiasa kieneo na kitaifa, ikiwa atachaguliwa kama mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Kinaya ni kwamba miezi michache iliyopita, kaka yake mkubwa Bw Odinga, Dkt Oburu Oginga, alimpendekeza Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa, Opiyo Wandayi, kuwa mrithi wa Bw Odinga.
Hali hiyo imezua mjadala mkali kuhusu kiongozi anayefaa kuchukua nafasi ya Bw Odinga, hasa uongozi wa ODM na ngome yake ya Luo Nyanza.
Mbali na Nyanza, mdahalo huo umekuwa ukiendelea katika maeneo ya Ukambani, Pwani na Magharibi, ambayo ni miongoni mwa ngome zake za kisiasa.
Hata hivyo, mjadala huo umeshika kasi sana katika eneo la Nyanza, ikizingatiwa kuwa hakujawahi kuwa na mazungumzo ya wazi kuhusu ni kiongozi yupi anayefaa kuwa mrithi wake.
Katika maeneo ya Ukambani, Pwani na Magharibi, tayari kuna viongozi wa kisiasa walioonyesha nia ya kumrithi Bw Odinga, wakiwemo kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, magavana wa zamani Hassan Joho (Mombasa) na Wycliffe Oparanya (Kakamega) mtawalia.
Kutokana na hali hiyo, wadadisi wanasema kuwa ikiwa Bw Odinga atajiuzulu kwenye ulingo wa siasa, basi mchakato wa urithi wake utakuwa wa kuvutia.
“Raila ni Mkenya, wala si wa kwanza kutafuta kazi nje ya nchi. Alisema kwamba ana wanawe wenye uwezo hapa, wanaoweza kuchukua nafasi yake. Bw Mbadi ni mmoja wao. Ninadanganya? Kwa miaka hiyo yote ambayo (Baba) amekufunza, bado unahitaji mafunzo mengine? Je, huna uwezo? Hapo ndipo roho ya ‘Baba’ ipo. Nimetoa tu kidokezo na anajua hivyo,” akasema Bi Idah, alipohutubu katika eneo la Nyandiwa, Suba Kusini, eneobunge anakotoka Bw Mbadi.
Mwaka uliopita, Dkt Oburu alianzisha mdahalo huo, baada ya kutoa kauli kwamba huenda Bw Odinga akajiondoa kwenye ulingo wa siasa.
“Viongozi huchipuka kama uyoga. Huwa wanachipuka kama uyoga na hivyo ndivyo Bw Wandayi amechipuka wala hakuna jambo lolote litakalomzuia kutwaa uongozi kwani tumemwachia. Hawa ndio watu watakaotupa mwongozo,” akasema Dkt Oginga kwenye hafla moja iliyofanyika katika eneo la Ugunja, Kaunti ya Siaya, Septemba mwaka uliopita.
Ijapokuwa Dkt Oginga alimdokeza Bw Wandayi kama kiongozi anayefaa zaidi kuchukua nafasi ya Bw Odinga, kuna viongozi wengine ambao wamependekezwa, hali inayoonekana kuzua ushindani mkali.
Bw Odinga alisisitiza kuwa hata akichaguliwa kinara wa AUC, ataendelea kuisaidia jamii hiyo. Ikiwa atatwaa nafasi hiyo, Bw Odinga alisema “atachukua mapumziko ya muda kutoka ulingo wa siasa ili kuelekeza juhudi zake katika kuitumikia Afrika.”
Wanasiasa wengine ambao wametajwa kumezea mate nafasi ya urithi ni Mbunge Babu Owino, Gavana Gladys Wanga na gavana wa zamani Evans Kidero.
“Hakuna lolote linalonizuia kurejea kwenye ulingo wa siasa, ikiwa hali itaniruhusu,” akasema, huku akisisitiza kuwa “uongozi wa kisiasa ni wa kugawiana majukumu.”
“Hata ikiwa sitakuwepo, kuna watu walio karibu nami walio tayari kuiongoza ODM na Azimio la Umoja,” akasema, bila kumtaja kiongozi ambaye angependa awe mrithi wake.
Bw Mbadi, kwa upande wake, aliwarai wakazi wa Nyanza kutosumbuliwa na nia ya Bw Odinga kuwania nafasi ya uenyekiti katika AUC.