IEBC: Wanne kifua mbele kumrithi Chebukati
MCHAKATO wa kuajiri mwenyekiti mpya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) umeripotiwa kufikia hatua ya mwisho wagombea wanne wakiwa kifua mbele huku kamati ya uteuzi ikikimbizana na muda ili kukamilisha mchakato kwa wakati.
Vyanzo kadhaa ndani ya kamati ya uteuzi ya IEBC inayosaka mwenyekiti na makamishna wa tume ya uchaguzi viliiambia Taifa Leo kwamba Bw Erastus Edung Ethekon (Turkana), Bw Abdulqadir Lorot Ramadhan (Baringo), Bi Anne Amadi (Homabay) na Bw Charles Nyachae (Kisii) ndio wanaoongoza kati ya wagombea 11 waliohojiwa kwa wadhifa wa mwenuyekiti.
“Wagombea hawa wanne waliongoza katika mahojiano ya wadhifa wa mwenyekiti wa IEBC kutoka kwa jumla ya watu 11 tuliowahoji. Bila shaka tutachagua majina mawili kati ya hawa wanne na kuyawasilisha kwa rais, ambaye atateua mmoja kisha atawasilisha jina hilo kwa Bunge la Kitaifa,” alisema mmoja wa wanachama wa kamati ya uteuzi.
Ripoti hii ilithibitishwa pia na mwanachama mwingine wa kamati.
Kamati ya uteuzi ya IEBC yenye wanachama tisa, inayoongozwa na Dkt Nelson Makanda, inatarajiwa kukamilisha mahojiano ya wanachama wa IEBC leo Alhamisi.
Mbali na uchaguzi mkuu wa 2027, tume hiyo inahitajika kuwa kazini haraka iwezekanavyo ili kushughulikia mipaka ya uchaguzi iliyocheleweshwa na chaguzi ndogo kadhaa.
Taifa Leo imebaini kuwa kati ya wagombea wanne, chama cha Bw Raila Odinga (ODM) kinapendelea IEBC inayoongozwa na aidha Bw Ethekon, mwenye umri wa miaka 48 ambaye ni wakili, au Bw Ramadhan, ambaye kwa sasa ni Hakimu Mkuu katika Mahakama ya Naivasha.
Hata hivyo, chama cha Rais William Ruto, UDA, kinapendelea hima Bi Amadi, mwenye umri wa miaka 60 na ambaye alikuwa Msajili Mkuu wa Idara ya Mahakama, au Bw Nyachae, mwenye umri wa miaka 67, aliyewahi kuwa mwenyekiti wa Tume ya Utekelezaji wa Katiba ya mwaka 2010 (CIC).
“Chama chetu cha ODM kilitia saini ushirikiano na serikali ya UDA inayoongozwa na Rais Ruto. Tunaendelea na mazungumzo kuhusu umuhimu wa kumteua Bw Ethekon au Bw Ramadhan kuongoza tume hiyo,” alisema afisa wa cheo cha juu wa ODM.
“Bw Ethekon na Bw Ramadhan ni vijana na wana uwezo wa kufanya kazi vizuri, kama walivyodhihirisha wakati wa mahojiano. Bi Amadi na Bw Nyachae tayari wamehudumu katika utumishi wa umma, hivyo ni haki pia wengine wapate nafasi ya kuhudumu,” afisa huyo aliongeza.
Bw Ramadhan ndiye aliyekuwa wa kwanza kuhojiwa na kamati ya Dkt Makanda kwa wadhifa wa mwenyekiti wa IEBC mnamo Machi 24, 2025, akifuatiwa na Bi Amadi, Bw Nyachae, na Bw Edward Katama Ngeywa (Trans Nzoia).
Bw Ethekon alihojiwa siku ya pili ya mahojiano, akitanguliwa na Bw Francis Kakai Kissinger (Vihiga), Jacob Ngwele Muvengei (Kitui), na Bi Joy Brenda Mdivo (Nairobi).
Sehemu ya 3 (4) ya Ratiba ya Kwanza ya Sheria ya IEBC inasema kwamba baada ya mahojiano, kamati ya uteuzi itachagua watu wawili waliotimiza sifa kuwa mwenyekiti na wengine tisa wenye sifa kuwa wanachama wa IEBC, na kisha kuwasilisha majina hayo kwa Rais.
Rais, kutoka kwa orodha hiyo, atateua mtu mmoja kuwa mwenyekiti na wengine sita kuwa wanachama wa tume hiyo.
Sheria pia inamtaka Rais, ndani ya siku saba baada ya kupokea majina kutoka kwa kamati ya uteuzi, kuyawasilisha kwa Bunge la Kitaifa kwa mujibu wa Sheria ya Uidhinishaji wa Uteuzi wa Umma.