Habari za Kitaifa

IEBC yakaribia kuiva Ruto akipokea majina ya walioteuliwa na jopo

Na MOSES NYAMORI May 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto anatarajiwa kuwasilisha majina ya walioteuliwa kuhudumu katika Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kwa Bunge la Kitaifa ndani ya siku saba kuidhinishwa.

Jumanne, Rais alipokea orodha ya walioteuliwa kutoka kwa Jopo la Uteuzi la IEBC, hatua inayokamilisha mchakato mrefu na mgumu wa kupata timu mpya itakayosimamia Uchaguzi Mkuu wa 2027.

“Asubuhi ya leo, nimepokea ripoti ya mchakato wa uteuzi wa walioteuliwa kwa wadhifa wa Mwenyekiti na Makamishna wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka kutoka kwa Jopo la Uteuzi la IEBC, katika Ikulu ya Nairobi,” alisema Rais.

“Kulingana na masharti ya Sheria ya IEBC, nitawasilisha majina hayo kwa Bunge la Kitaifa nikiwa mwaminifu kikamilifu kwa misingi ya kikatiba inayoongoza utawala wetu,” aliongeza.

Jopo hilo la watu tisa, likiongozwa na Dkt Nelson Makanda, lilihoji wawaniaji 11 kwa wadhifa wa Mwenyekiti wa IEBC na wengine 107 waliomezea mate kuwa makamishna

Kwa mujibu wa Sheria ya IEBC, Rais anapaswa kuwasilisha orodha ya walioteuliwa kwa Bunge kuidhinishwa ndani ya siku saba. Baada ya kuidhinishwa na Bunge la Kitaifa, Rais atakuwa na siku nyingine saba kuteua rasmi Mwenyekiti na makamishna wa tume hiyo.

IEBC imekuwa haifanyi kazi kwa zaidi ya miaka miwili kufuatia kustaafu kwa Mwenyekiti wa zamani Wafula Chebukati na makamishna wawili wengine, Boya Molu na Abdi Guliye mnamo Januari 2023.

Hata hivyo, hata kabla ya kumalizika kwa muda wa Chebukati, matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2022 yaliigawanya tume hiyo katikati.

Makamishna wanne – Bi Juliana Cherera (Makamu Mwenyekiti), Bw Justus Nyangaya, Francis Wanderi na Bi Irene Masit – maarufu kama “Cherera Four”  walikataa ushindi wa Rais Ruto. Dkt Ruto alimshinda kiongozi wa upinzani Raila Odinga kwa tofauti ndogo.

Baada ya Dkt Ruto kuingia madarakani, makamishna hao wanne waliondolewa kwa kishindo. Walishutumiwa kwa kumpendelea Bw Odinga kwa kushinikiza uchaguzi wa marudio ili kuzuia kutangazwa kwa Dkt Ruto kama Rais.

Madai yaliwasilishwa bungeni yalitaka Rais kuunda tume ya uchunguzi kuwachunguza makamishna hao kwa madai ya kupinga matokeo ya urais.

Pia walishutumiwa kwa kujaribu kubadilisha matokeo ya urais ili kuilazimisha nchi kufanya uchaguzi wa marudio kati ya Dkt Ruto na Bw Odinga.

Bunge la Kitaifa lilikubali ripoti ya Kamati ya Sheria na Haki, iliyopendekeza kuundwa kwa tume ya uchunguzi.

Uamuzi huo uliwafanya Bi Cherera, Bw Nyangaya na Bw Wanderi kujiuzulu.

Bi Masit alikabili tume hiyo ambayo baadaye ilipendekeza aondolewe ofisini.