Habari za Kitaifa

IEBC yapewa siku saba kujibu kesi ya kutimua wabunge

Na JOSEPH WANGUI August 9th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mahakama Kuu imepatia Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) muda wa siku saba kujibu kesi kuhusu madai ya kukataa kushughulikia maombi ya kutimua wabunge kutoka afisini.

Katika maagizo yaliyotolewa na Jaji Chacha Mwita, mahakama pia imepatia Mwanasheria Mkuu na Bunge la Kitaifa muda sawa wa siku saba kuwasilisha majibu ya kesi iliyowasilishwa na wapiga kura sita.

Jaji Mwita alitoa maagizo hayo baada ya kuwakataa ombi la dharura la wapiga kura hao aamuru IEBC ianze mara moja kushughulikia maombi ya wananchi ya kutaka kuwatimua wabunge.

Wapiga kura hao walitaka mahakama itoe amri ya muda kuagiza IEBC kushughulikia maombi ya wananchi wanaotaka kuondoa baadhi ya wabunge kutoka nyadhifa zao.

Hata hivyo, Jaji Mwita aliwaagiza wawasilishe stakabadhi za kesi kwa IEBC, Mwanasheria Mkuu na Bunge la Kitaifa, na wahakikishe majibu yote yamewasilishwa ndani ya siku saba baada ya kupeleka stakabadhi hizo. Pia pande zote ziliagizwa kuandaa na kubadilishana hoja zao kwa maandishi.

Wapiga kura hao sita ni Newton Mugambi Boore, Dennis Mwaki Chabari, Morris Mawira, Agnes Mwende Justus, Seth Mark Kinoti na Christine Kanana Kithinji.

Walisema kwamba IEBC imekiuka Katiba kwa kukataa kushughulikia maombi ya wananchi ya kuwataka baadhi ya wabunge waondolewe madarakani.

Kwa mujibu wa kesi hiyo, IEBC na Bunge la Kitaifa zimeendelea kukataa kutekeleza masharti ya wazi ya Ibara ya 104 ya Katiba inayohusu haki ya wananchi kumwondoa mbunge kabla ya kipindi cha uchaguzi kukamilika.

“Ibara hiyo inawapa wananchi mamlaka ya kuondoa wabunge waliowachagua iwapo watashindwa kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” walisema walalamishi.

Katika kesi hiyo, IEBC ilieleza kuwa hakuna sheria inayotoa mwongozo wa jinsi ya kumwondoa mbunge wa Bunge la Kitaifa au Seneti na hivyo haiwezi kushughulikia maombi hayo.

Hata hivyo, wakili Muriuki Muriungi anayewakilisha wapiga kura hao, anasema IEBC inatumia mwanya wa kimakusudi uliotengenezwa na Bunge la Kitaifa kama kisingizio.

Anadai kuwa kuna uzembe wa makusudi kutoka kwa Bunge, na kwamba kutotekelezwa kwa kifungu cha Katiba ni sawa na kusimamishwa kwa Haki za Kimsingi za Wananchi.

Alisema uamuzi wa IEBC kukataa kushughulikia maombi ya kuwatimua wabunge umewanyima Wakenya fursa ya kuwawajibisha viongozi waliokosea au waliokiuka Katiba.

Kwa upande wa Bunge, alisema kukataa kuanzisha sheria inayowezesha mchakato wa kuwawajibisha wabunge ni sawa na kusimamisha utekelezaji wa Ibara ya 104 ya Katiba.

Wakili Muriungi anasema wateja wake wanaamini kuwa haki ya kuwatimua wabunge ni zana muhimu ya uwajibikaji na kwamba kukosekana kwa sheria hiyo ni ushahidi tosha kuwa wabunge hawataki kuwajibika kwa wapiga kura wao.

“Wabunge wameamua kusimamisha utekelezaji wa Katiba ili kuwazuia wapiga kura wa maeneo yao kuwatimua kwa sababu ya makosa makubwa au utendakazi mbaya,” alisema.

Aliongeza kuwa ni jambo la kushangaza kuwa katika mwaka wa 2020, wabunge walibadilisha Sheria ya Serikali za Kaunti ya mwaka 2012 na kuweka mfumo wa wazi wa kuwaondoa Madiwani, lakini hawakufanya vivyo hivyo kwa wabunge.

“Madiwani na Wabunge wote wanafanya kazi ya kutunga sheria na kuwasimamia viongozi wengine katika viwango tofauti vya serikali, hakuna sababu ya kumwezesha mwananchi kumtimua diwani na kumlinda Mbunge,” alisema wakili huyo.