Habari za Kitaifa

Ikiwa wewe ni mwalimu wa sayansi na unatafuta kazi, TSC inakutafuta

Na MARY WANGARI October 24th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

TUME ya Kuajiri Walimu (TSC) imekiri kwamba kuna uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi huku mchakato wa kuajiri walimu wanagenzi ukitazamiwa kung’oa nanga rasmi Januari mwaka ujao.

Afisa Mkuu Mtendaji wa TSC Nancy Macharia, alieleza Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Elimu Jumatano kuwa, “licha ya kuandikia Wizara ya Elimu mara kadhaa kuhusu suala hilo na kutangaza nafasi za kazi kwa walimu wa sayansi, hakuna maombi yanayotumwa.

“Ni sharti tukubali kuwa tuna uhaba wa walimu wa sayansi. Idadi kubwa ya walimu wanaofuzu kutoka vyuo vikuu ni wa masomo ya sanaa. Huwa hatupati walimu wa sayansi tunapotangaza,” Bi Macharia alieleza wabunge.

“Tunatangaza nafasi za kazi kwa walimu wa fizikia na hatupati yeyote.”

Wabunge walielezea wasiwasi wao kwamba uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi umewalazimu walimu wa masomo ya sanaa kutwikwa jukumu hilo hali inayoishia kuathiri wanafunzi.

“Hali iliyopo mashinani ni kuwa walimu wa masomo ya sanaa wanafunza sayansi. Wanachofanya ni kuwa, wanasoma usiku kisha wanakuja kukariria wanafunzi mchana. Huko ni kufunza,” alihoji Mbunge wa Kabondo Kasipul, Eve Obara.

Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Tinderet, Julius Melly, ilisikia kuwa walimu zaidi ya 400,000 bado hawajaajiriwa nchini.

Jumla ya walimu 314.117, walituma maombi ya kazi kwa nafasi 46,000 zilizotangazwa za walimu wa Sekondari Msingi (JSS), alieleza Bi Macharia.

Mkuu huyo wa TSC alisema kuwa shule za walemavu zina uhaba wa walimu 5,358.