Habari za Kitaifa

IPOA yataka polisi wachukuliwe hatua za kinidhamu kuhusu shambulizi dhidi ya Gachagua Nyandarua

Na WAIKWA MAINA January 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MAMLAKA Huru ya Kuchunguza Utendakazi wa Polisi-IPOA imependekeza hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi ya maafisa wakuu wa polisi wa Nyandarua kwa utovu wa nidhamu kitaaluma wakati aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua alishambuliwa katika maombi ya madhehebu mbalimbali huko Shamata.

Washirika wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua wanasema kuwa hatua za kinidhamu za ndani zilizopendekezwa na IPOA hazitoshi na kwamba maafisa hao wanapaswa kushtakiwa kwa makosa ya uhalifu mahakamani.

Wakati wa tukio hilo katika Uwanja wa Shamata, afisa wa polisi kutoka Kituo cha Polisi cha Athi River alirusha kitoa machozi kwenye jukwaa kumlenga Gachagua, wageni na mapasta.

Katika taarifa yake, IPOA inawalaumu wakuu wa polisi jinsi walivyoshughulikia tukio hilo tangu waandalizi walipopanga hafla hiyo hadi kufikia hatua ya kuvurugwa, jambo linaloashiria kwamba polisi walikuwa na nia mbaya katika tukio zima.

“Mnamo Desemba 28, 2024, hafla ya maombi katika Uwanja wa Shamata katika Kaunti ya Nyandarua ilitatizwa wakati kitoa machozi kiliporushwa kwenye jukwaa. Mshukiwa huyo, anayeripotiwa kuwa afisa wa polisi, alishambuliwa na umma, kabla ya kuokolewa na polisi. IPOA ilifuatilia shughuli hiyo ili kutoa mapendekezo na ushauri kwa hatua zaidi,” inasema sehemu ya taarifa ya IPOA iliyotolewa Januari 2, takriban siku tano baada ya tukio hilo.

Ripoti ya IPOA inaeleza kuwa kamati ya usalama ya Kaunti Ndogo ya Aberdare hapo awali ilifuta hafla hiyo, lakini ikaidhinisha siku moja kabla ya tukio hilo, na kwamba walituma angalau maafisa 60 wa polisi bila agizo rasmi la jinsi ya kutekeleza operesheni.

“Kamanda wa Polisi wa Kaunti aliongoza operesheni hiyo lakini hakuweka uwepo wake katika Kitabu cha Matukio cha kituo hicho. Washukiwa watano walikamatwa asubuhi kwa kupanga kutatiza tukio hilo lakini baadaye waliachiliwa kwa maagizo kutoka kwa Kamanda wa Polisi wa Kaunti hiyo. Maelezo ya washukiwa walioachiliwa hayakurekodiwa kikamilifu katika Kitabu cha Matukio, na hivyo kuibua wasiwasi wa uwajibikaji,” inasema sehemu ya taarifa hiyo.

Mamlaka inabainisha kuwa kisa hicho cha vitoa machozi kilizua hofu seneta mmoja alipokuwa akitoa hotuba yake.

IPOA inasema afisa wa polisi aliyerusha kitoa machozi alipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Ndaragua, takriban kilomita 30 kutoka eneo la tukio, kwa siri, na kisha kuachiliwa bila kurekodi katika Kitabu cha Matukio.

“Kitengo cha Masuala ya Ndani (IAU) na Mamlaka Huru ya Kusimamia Polisi (IPOA) zilichunguza kuachiliwa kwa mshukiwa kwa njia isiyoeleweka na kushughulikiwa kwa kesi hiyo na polisi na kuhitimisha yafuatayo. Polisi walishindwa kushughulikia kukamatwa kwake na mchakato wa kuachiliwa kwa mtuhumiwa kitaaluma. Licha ya kuwa na habari za ujasusi kuhusu uwezekano wa kutokea kwa ghasia, hakuna Agizo la Operesheni lililotayarishwa kwa mpangilio wa usimamizi wa umma katika hafla hiyo. Kuachiliwa kwa afisa wa polisi aliyeshukiwa bila uchunguzi na uwezekano wa matumizi mabaya ya mamlaka na polisi,” IPOA inasema.

Ripoti hiyo inaongeza: “IPOA ilifanya uchunguzi wa kina kuhusu utepetevu wa polisi na utovu wa nidhamu na kupendekeza kwamba hatua zichukuliwe kwa maafisa waliohusika katika kushughulikia tukio hilo isivyofaa.”

Seneta John Methu anasema hatua za ndani za kinidhamu hazitoshi kwani tukio hilo lilipangwa vyema kusababisha fujo na kuwadhuru watu.

“Hatua za ndani za kinidhamu zimependekezwa dhidi ya afisa wa polisi lakini hiyo haimzuii kuwajibika kama mhalifu aliyetishia maisha katika hafla ya umma kwa hivyo ni lazima afikishwe kortini,” Seneta Methu alisema.