Habari za Kitaifa

Jaji Koome: Sitazami runinga kwa sababu ya visa vya Wakenya kuhangaika vinavyonikwaza  

Na WYCLIFFE NYABERI August 23rd, 2024 Kusoma ni dakika: 2

JAJI Mkuu, Martha Koome amesema hatazami habari za runinga kwa sasa kwa sababu ya kukwazika kufuatia mahangaiko yanayokumba Wakenya ‘anayoamini yanaweza kuangaziwa’.  

Rais huyo wa Idara ya Mahakama amesema alichukua hatua hiyo, ili kuepuka visa vya kuvunja moyo, vinavyomkumbusha kuhusu ukosefu wa usawa katika jamii.

Akiongea mnamo Alhamisi, Agosti 22, 2024, Bi Koome alitumia mfano mfumo wa sasa wa kutoa ufadhili wa elimu kwa wanafunzi wa Vyuo Vikuu kama mojawapo ya visa vinavyomchukiza kufuatilia habari.

Akionekana kuukejeli mfumo huo, Bi Koome alisema alikuwa akisikitishwa na habari za wanafunzi maskini ambao walikuwa wakilalamika kuwa wamewekwa kwenye ngazi ambazo ni za watu matajiri.

“Niliacha kutazama habari kwa sababu ya habari ambazo zinazidi kuangaziwa machoni petu kutukumbusha kuhusu ukosefu wa usawa katika jamii. Mwanafunzi aliyefuzu kwenda Chuo Kikuu, anaangaziwa akilia kuwa amewekwa kwenye bendi ya tano ilhali anafaa kuwa katika bendi ya kwanza. Ukifuatilia, unapata ya kwamba mtoto katika familia inayojiweza, amewekwa katika bandi au ngazi ya kwanza,” Bi Koome alilalama.

Badala ya mfumo huo wa sasa ambao umewafanya Wakenya wengi kuelezea kutoridhishwa nao, Jaji Mkuu alisema elimu yote inafaa kufanywa kuwa bure kwa Wakenya.

Bi Koome aidha alihoji jinsi basari za viongozi mbalimbali hutolewa na kusema kuwa pesa hizo zinafaa kuelekezwa kwa Wizara ya Elimu ili kufanya masomo kuwa ya bure.

“Kunazo basari ambazo hupewa magavana, Wawakilishi wa Kike, wabunge kupitia hazina ya Ustawishaji wa Maeneobunge na madiwani. Pesa katika basari hizi hupeanwa vipi? Mbona fedha hizo zisiwekwe katika Wizara ya Elimu na masomo yawe ya bure?” Bi Koome aliuliza.

Mfumo wa sasa wa kutoa ufadhili kwa elimu ya Vyuo Vikuu umegawanywa katika makundi matano.

Kundi la kwanza ni la watu wachochole sana na kundi la tano ni la mabwanyenye.

Kufuatia malalamishi ya wazazi kuhusu kuratibiwa kwa wanafunzi katika ngazi hizo visivyo, Waziri wa Elimu Migos Ogamba aliviamuru Vyuo Vikuu kuwasajili wanafunzi wa mwaka wa kwanza bila kujali ikiwa wamelipa karo wanayohitajika mara moja au la.

Waziri Ogamba aliwataka wanafunzi walioratibiwa katika ngazi ambazo hawafai kukata rufaa ambazo alisema zitashughulikiwa ndani ya kipindi cha wiki tatu.

Hata hivyo, Waziri Ogamba hakueleza kama mfumo huo mpya utatupiliwa mbali.

Tayari wabunge wameutaja mfumo huo mpya kama unaokandamiza na kutaka utupiliwe mbali.