Kindiki atangaza kiama kwa mafisadi serikalini baada ya Rais kuidhinisha sheria mpya
MAWAZIRI, Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na maafisa wengine wa Idara ya Mahakama pamoja na Wawakilishi Wadi (MCA) sasa watalazimika kutangaza mali zao kama sehemu ya juhudi mpya za Rais William Ruto za kupambana na ufisadi.
Hatua hii inafuatia kutiwa saini kwa Mswada wa Mgongano wa Maslahi wa 2025 kuwa sheria na Rais katika Ikulu jana, baada ya zaidi ya miaka miwili ya mvutano kati ya Bunge na Afisi ya Rais.
Sheria mpya inazuia upendeleo na ushawishi wa nje katika kandarasi zinazohusiana na majukumu ya afisa wa umma.
Zaidi ya hayo, sheria hii inatambua Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kama afisi ya serikali inayowajibika kwa kushughulikia masuala yote yanayohusu mgongano wa maslahi, kulingana na Kifungu cha 79 cha Katiba.
Kifungu hicho kinaitaka EACC kuhakikisha utekelezaji wa masharti ya Sura ya Sita ya Katiba kuhusu uongozi na uadilifu, ikiwa ni pamoja na kuepuka mgongano wa maslahi.
Kuhusu kutangaza mali, sheria mpya inapanua maafisa wa umma na wa serikali wanaotakiwa kutangaza mali zao, ambao awali hawakuwa wamejumuishwa katika Sheria ya Maadili ya Maafisa wa Umma, ambayo sasa imebatilishwa.
Wanaojumuishwa sasa ni pamoja na Wawakilishi Wadi na maafisa wa Idara ya Mahakama, akiwemo Jaji Mkuu, Naibu Jaji Mkuu na wengine.
Maafisa wa serikali na wa umma watalazimika kuwasilisha maelezo kuhusu mali kila baada ya miaka miwili kwa taasisi inayosimamia shughuli hiyo, chini ya usimamizi wa EACC.
Tangazo hilo litajumuisha mapato, mali na madeni yao, pamoja na ya wake wao na watoto wanaowategemea.
Kwa upande wa mgongano wa maslahi, sheria mpya inamzuia afisa wa umma kupendelea mtu yeyote kinyume na sheria au sera iliyoandikwa, au kushawishiwa na ahadi za ajira kutoka nje katika utekelezaji wa mamlaka au majukumu rasmi.
Vilevile, sheria inakataza afisa wa umma kuingia katika mikataba ya kusambaza bidhaa au huduma na taasisi anayofanyia kazi au kuwa na ushawishi kuihusu.
Sheria pia inakataza afisa wa umma kumiliki hisa katika kampuni au shirika lolote la kisheria lililo na mkataba na taasisi anayohudumia.
Aidha, sheria hii inapiga marufuku ajira nyingine yoyote ya kibiashara inayokinzana na majukumu ya afisa wa umma au inayoathiri uamuzi wake wa kitaaluma, na hivyo kusababisha mgongano wa maslahi.
Akizungumza wakati wa hafla ya kutiwa saini kwa mswada huo kuwa sheria, Rais Ruto alisema kuwa sheria hiyo itakomesha matumizi mabaya ya mamlaka na kuhakikisha kuwa rasilmali za umma zinatumika kwa makusudi yake.
Rais alisema sheria hiyo mpya inaweka kanuni wazi kuhakikisha maafisa wa umma wanahudumu kwa uadilifu, uwazi na uwajibikaji.
Alisema sheria hiyo pia inawapa Wakenya fursa ya kuwawajibisha maafisa wa umma wanapotumia mamlaka yao vibaya.
“Hili ni tukio muhimu sana kwa Kenya. Tumeziba mianya ya watu kutumia nyadhifa zao kwa manufaa ya kibinafsi,” alisema Rais Ruto.
“Kwa EACC, sasa mna nyenzo za kulinda rasilmali za Jamhuri ya Kenya na kuwajibisha kila afisa wa umma,” aliongeza.
Naibu Rais Kithure Kindiki alisema kuanza kutekelezwa kwa sheria hiyo ni pigo kubwa kwa ufisadi.
Alisema sheria hiyo mpya inafunga mianya ambayo maafisa wafisadi walikuwa wakitumia kuiba fedha za umma, na inawazuia kutumia vibaraka kufanikisha ufisadi.
“EACC sasa ina mamlaka makubwa ya kupambana na ufisadi, matumizi mabaya ya mamlaka na udanganyifu wa imani ya umma kwa manufaa ya kibinafsi,” alisema Profesa Kindiki.