Habari za Kitaifa

Jaji Njoki Ndung’u akimbilia korti imuokoe asiondolewe ofisini

Na JOSEPH WANGUI February 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

JAJI wa Mahakama ya Juu zaidi nchini Njoki Ndung’u ameelekea katika Mahakama Kuu kuzuia kuondolewa kwake afisini kutokana na pendekezo la aliyekuwa Waziri Raphael Tuju na wakili Nelson Havi.

Katika stakabadhi zilizowasilishwa mahakamani na wakili Andrew Musangi, Jaji Ndung’u amewasilisha kesi dhidi ya Tume ya Huduma za Mahakama (JSC) akisema mchakato unaoendelea hapo huenda ukaishia kuondolewa kwake afisini na kuundwa kwa jopo la kuchunguza mienendo yake na majaji wenzake wa Mahakama ya Juu Zaidi.

Anataka JSC izuiliwe kushughulikia maombi yaliyowasilishwa dhidi yake na majaji wengine sita wa mahakama hiyo, akiwemo Jaji Mkuu Martha Koome.

Japo JSC inashughulikia maombi matatu yaliyowasilishwa na kampuni ya Dari Limited inayomilikiwa na Tuju, Bw Havi na wakili Christophet Rosan, stakabadhi za mahakama zinaonyesha kuwa Jaji Njoki hapingi ombi lililowasilishwa na mlalamishi wa tatu.

Bw Tuju na Bw Haki, pamoja na Bw Rosana wameitaka JSC iwafute kazi majaji wote saba wa Mahakama ya Juu kwa utendakazi mbaya na utovu wa maadili walipokuwa wakishughulikia kesi mbalimbali.

Jaji Njoki anataka Mahakama Kuu iamuru kusitishwa kwa JSC kushughulikia maombi hayo hadi kesi aliyoiwasilisha itakapoamuliwa.

Anataja mchakato unaoendelezwa kwa nia ya kumwondoa afisini kama “unaokiuka Katiba na usio na msingi wowote.”

Jaji Njoki anaeleza kuwa shughuli zinazoendelea katika JSC kuhusiana na maombi hayo zinahalalisha mamlaka ya majaji ya kutoa maamuzi na hivyo ni kinyume cha kipengele cha 160 cha Katiba kinacholinda uhuru wa Idara ya Mahakama.

Aidha, Jaji huyo anaamini kuwa hatua ya JSC inakwenda kinyume na kanuni ya kuwalinda majaji kutokana na kuingiliwa bila sababu.

Jaji Njoki pia anakosoa JSC kwa kupokea maombi hayo na kuyaorodhesha kusikizwa, akisema hilo likiruhusiwa kuendelea “watu wenye nia mbaya wataendelea kutumia JSC kama silaha za kuwasaidia kuendesha vita dhidi ya majaji kufanikisha malengo yao finyu.

“Huku Jaji Njoki akitambua na kuheshimu wajibu wa JSC katika kuendeleza uwajibikaji katika idara ya mahakama, ni wazi kuwa wajibu huo haujumuishi kubatilisha maamuzi ya majaji yanayotolewa wanapotekeleza majukumu yao,” akasema wakili Musangi.

Imetafsiriwa na Charles Wasonga