JANJA NA JANJAURE: Jinsi kutimua Gavana Mutai kulikita katika kuamua iwapo ilihitaji MCAs 31 au 31.3
GAVANA wa Kaunti ya Kericho, Erick Mutai, Jumatatu alinusurika jaribio la kumng’oa mamlakani katika muda wa miaka miwili pekee tangu alipochukua usukani.
Pingamizi kutoka kwa wakili Katwa Kigen, kuhusu iwapo Bunge la Kaunti ya Kericho lilitimiza kiwango cha thuluthi mbili kinachohitajika kumfurusha Gavana afisini lilichangia pakubwa kumwokoa mkuu huyo wa kaunti dhidi ya kurushwa nje.
Hii ni baada ya zaidi ya saa tano zilizojaa taharuki na muda wa chini ya dakika tano wa kupiga kura huku maseneta wakigawanyika kuhusu iwapo kiwango cha thuluthi mbili kilitimizwa ili kuruhusu ufurushaji.
Ili kuokoa muda, Naibu Kiongozi wa Wengi Bungeni ambaye ni Seneta wa Nakuru Tabitha Karanja aliwasilisha hoja iliyoungwa mkono na Kiongozi wa Wachache, Stewart Madzayo, kuunga mkono pingamizi hilo na kuzima mashtaka dhidi ya Gavana Mutai.
Spika Amason Kingi aliwaruhusu maseneta kupiga kura kuhusu suala hilo akisema ni maseneta wasiopungua 24 waliohitajika kuunga mkono hoja hiyo ili kukatiza vikao hivyo.
Maseneta 34 walipiga kura kuunga mkono hoja hiyo ikilinganishwa na 10 waliopinga na kumwokoa Gavana Mutai kisiasa.
“Hoja ikiwa imeidhinishwa, vikao vya kusikiza pendekezo la kumtimua Gavana wa Kericho Erick Mutai vimezimzwa…,” alisema Spika Kingi.
Kura zilizopigwa na seneta wake Aaron Cheruiyot, Samson Cherargey (Nandi), Boy Issa Juma (Kwale), Madzayo (Kilifi), Okong’o Omogeni (Nyamira), Oburu Oginga (Siaya), Tom Ojienda (Kisumu), Ledama Olekina (Narok), Mohamed Faki (Mombasa) na Enoch Wambua (Kitui) hazikuwa na athari kubwa.
Safari ya kumwokoa Gavana ilianza saa tano Wakili Kigeni aliposimama na kuirai Seneti kukatiza mashtaka dhidi ya mkuu huyo wa kaunti anayehudumu kwa mara ya kwanza kama gavana, wakisema viwango vinavyohitajika havikutimizwa.
Alihoji kuwa kiwango kinachohitajika ili kupitisha hoja ya kumng’atua afisini Dkt Mutai ni madiwani 32 ilhali ni 31 pekee waliopitisha hoja hiyo.
Akirejelea kesi zinazohusu utimuaji ikiwemo kuchaguliwa kwa Spika wa Bunge la Kaunti Dkt Patrick Mutai na kufurushwa kwa Gavana Paul Chepkwony, Wakili alisema ni wazi kwamba kiwango cha thuluthi mbili kinahitaji madiwani 32 miongoni mwa 47.
“Kiwango hicho hakifai kubadilika kwa sababu ni Gavana Mutai. Huo utakuwa ubaguzi,” alisema Bw Kigen.
“Hoja hiyo haijatimiza kiwango cha thuluthi mbili. Kwa bunge la kaunti ya Kericho ambalo lina madiwani 47 MCAs, thuluthi mbili inatimia ikiwa kura zinafika 31.3 wala si madiwani 31,” alihoji Bw Kigen.
Wakili wa Bunge la Kaunti Elias Mutuma alijaribu kupuuzilia mbali pingamizi hilo la awali akihimiza Seneti kuruhusu vikao kuendelea.
“Tutatoa ushahidi kuashiria kuwa viwango vinavyohitajika vilitimizwa. Ruhusu suala hili lisonge mbele kisha usaili ufaafu wa suala hili kupitia kuwahoji mashahidi,” alisema Bw Mutuma.