Habari za Kitaifa

Ni kuogopa ‘salamu’? Wabunge wapinga mswada unaotaka kuharamisha maandamano

Na SAMWEL OWINO December 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

WABUNGE wamepinga mswada unaolenga kudhibiti maandamano wakisema unaingilia haki ya kikatiba ya Wakenya.

Wanachama wa Kamati ya Bunge kuhusu Usalama pia wanasema mswada hamna mapya yanayopendekezwa kwenye mswada huo kwani mapendekezo yake yote yameshughulikiwa na Sheria ya sasa kuhusu Usalama wa Umma.

Baada ya kuukagua mswada huo, Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Narok Magharibi Gabriel Tongoyo ilimwambia mdhamini wa mswada huo kwamba kuwa mwangalifu asikanganyikiwe na kipengele cha 24 cha Katiba kinachoolezea mipaka ya haki na kipengele cha 37 kinacholinda haki ya raia kufanya maandamano.

Kulingana na Kipengele cha 37, “Ni haki ya kila raia kukongamana kwa amani, kufanya maandamano na kuwasilisha malalamishi kwa asasi za serikali.

Uhuru na haki ya kimsingi

Nacho kipengele cha 24 kuhusu mipaka ya kufurahishwa kufurahishwa kwa haki kinasema kuwa “uhuru au haki ya kimsingi katika sura kuhusu Haki ya Kimsingi haiwezi kudhibitiwa na sheria yoyote, isipokuwa ikiwa udhibiti huo unakubaliwa katika jamii ya kidemokrasia na kwa kuzingatia masuala yote husika.”

Idara ya kisheria ya kamati hiyo ilisema kuwa kile ambacho ni kipya katika mswada huo, uliodhaminiwa na Mbunge wa Mbeere Kaskazini Godffrey Ruku, ni uwepo wa maafisa wa kudhibiti waandamanaji.

“Hata hivyo, pendekezo hilo linaweza kufikiwa kwa kuifanyia mabadiliko Sheria ya Usalama wa Umma,” inasema taarifa ya idara hiyo.

Mbw Ruku alikuwa ameratibiwa kufika mbele ya kamati hiyo jana, lakini hakufika.

Kamati hiyo iliambiwa kuwa Mbunge huyo wa chama cha Democratic Party (DP) alikuwa amebanwa na shughuli zingine nje ya Nairobi.

Bw Tongoyo alisema kamati yake itaratibu mkutano mwingine na Bw Ruku ili kumfahamisha rasmi kuhusu uamuzi wa wanachama na idara ya sheria ya kamati hiyo.

Kumshauri mdhamini

“Tunapaswa kumshauri mdhamini wa mswada huu kwamba anahitaji kuuleta kama mswada wa marekebisho ya sheria iliyo. Tutatafuta nafasi ili tukutane na Mheshimiwa Ruku ili kumfahamisha rasmi kuhusu maoni ya kamati hii,” Bw Tongoyo akaeleza.

Mbunge wa Nyakach Aduma Owuor pia alisema baadhi ya mapendekeza kuwa baadhi ya mapendekezo kwenye mswada huo tayari yako kwenye Sheria ya Usalama wa Umma ilhali mapendekezo mapya yanaweza kuibua utata wakati wa utekelezaji.

“Itakuwa vigumu kutekeleza mapendekezo mapya yaliyoibuliwa na mbunge huyu kwenye mswada wake,” akasema Owuor.

“Nakubaliana kabisa na kauli kutoka idara ya sheria kwamba baadhi ya yale yanayopendekezwa na Bw Ruku tayari yako kwenye Sheria ya Usalama wa Umma,” akaongeza.

Wanachama wa kamati hiyo pia wanalalamika kuwa mswada huo, “The Assembly and Demonstration Bill 2024″, unaipa serikali mamlaka ya kuwazuia Wakenya kufurahia haki yao ya kidemokrasia inayolindwa na katiba.

IMETAFSIRIWA NA CHARLES WASONGA