Jinsi mkuu wa zamani wa KPA alilipa Sh1.4 bilioni kwa ujenzi wa matuta
MBUNGE wa Nyaribari Masaba Daniel Manduku alilipa kitita cha Sh1.4 bilioni kwa ujenzi wa matuta katika bandari ya Kilindini alipokuwa meneja mkurugenzi wa KPA, mahakama ya kuamua kesi za ufisadi imefahamishwa.
Akitoa ushahidi mbele ya hakimu mkuu Dkt Victor Wakumile, mkurugenzi wa Absam & Sun Limited Abdisalaam Hassan alisema ijapokuwa kandarasi hiyo iliidhinishwa 2016 ujenzi ulifanyika 2019.
Bw Hassan alisema Bw Manduku aliidhinisha alipwe Sh82 milioni.
Katika ushahidi uliowasilishwa mbele ya Bw Wakumile, Bw Manduku alilipa pesa ambazo hazikuwa zimetengewa ujenzi wa matuta kipindi cha matumizi ya pesa cha 2018/2019.
Bw Hassan aliambia mahakama kwamba zabuni ya ujenzi wa matuta katika bandari ya Kilindini haikuwa na tarehe na wala haikuwa imeonyesha kiwango cha pesa ambacho kilitengwa kutumika.
Manduku amekana shtaka la kutumia vibaya mamlaka ya afisi na kuidhinisha malipo ya Sh1.4 bilioni kinyume cha sheria.
Manduku ameshtakiwa pamoja Fadhili Juma anayeshtakiwa kulipa zaidi ya Sh244 milioni kinyume cha sheria.
Wamekanusha mashtaka dhidi yao na wako nje kwa dhamana.