Jinsi tulivyolipwa kumuua aliyekuwa Waziri Tom Mboya
TULIPOWASILI nyumbani kwake Runyenjes, Kaunti ya Embu, Ndwiga Kathamba Muruathika, almaarufu ‘Ndume’, ndipo alikuwa ameamka.
Ndigwa, 92, ni mzee ambaye ameshuhudia mengi nchini kuanzia harakati za kupigania uhuru wa Kenya hadi tawala za marais watano wa Kenya.
Baada ya kutukaribisha katika boma lake, anarejea ndani ya nyumba kisha anamwita mwelekezi wetu, Moses Wamuru, kwa mazungumzo mafupi.
Tunaposubiri nje, tunajiandaa kwa mahojiano.
Baada ya muda mfupi Mzee Ndwiga anatokea akiwa amevalia suti nyeusi na shati nyeupe, akiandamana na dada zake wawili.
Anauliza kile tunataka kutoka kwake kisha anaketi.
Ghafla bin vuu, Ndwiga anapasua mbarika kwamba ni miongoni mwa vijana watatu wa Kanu waliolipwa na mtu ambaye hangemtaja jina, kutokana na kiapo cha usiri walicholishwa kutekeleza mauaji.
Anasema walipewa kibarua cha kumfuatilia aliyekuwa Waziri wa Mipango ya Kiuchumi na Maendeleo ya Kitaifa Tom Mboya hadi siku alipopigwa risasi katikati mwa jiji la Nairobi Jumamosi Julai 5, 1969.
Mboya aliuawa alipokuwa akiondoka duka la dawa katika barabara ya Moi karibu na jumba la kuhifadhi kumbukumbu National Archives.
Mzee huyo, ambaye akili zake zingali timamu licha ya umri wake mkubwa, anafichua huku akibana maelezo.
Ndwiga anashikilia kuwa bado anabanwa na kiapo cha usiri alicholishwa miongo kadha iliyopita na hivyo hawezi kufichua mengi.
Lakini kwa upande mwingine, anasema hataki kuenda kaburini na baadhi ya siri chafu ambazo ameficha kwa miaka 55.
Mzee Ndwiga anadai siri hizo ni mzigo ambao ameubeba na anataka kuuachilia.
Kulingana na Mzee huyo, yeye na wenzake wawili (Vijana wa Kanu wakati huo) walijumuishwa katika njama ya kumuua Mboya miezi sita mapema, Januari 1969.
Wawili hao walikuwa Nahashon Njenga kutoka iliyokuwa wilaya ya Kiambu na Gitonga Gathanju kutoka Nyeri.
Ndwiga alikuwa kijana wa Kanu aliyewakilisha Embu.
Baadaye Njenga alishtakiwa kwa mauaji ya Mboya na kuhukumiwa kunyongwa.
Mzee huyu anasema walikuwa sehemu ya kundi ambalo lilipelekwa Bulgeria kwa mafunzo ya kijeshi na walijuana na Mboya ambaye alishikilia wadhifa wa Katibu Mkuu wa Kanu.
Ndwiga anadai mipango ya kumuua Mboya iliibuliwa na kundi la maafisa wenye ushawishi mkubwa serikalini na waliotoka Kiambu.
Lakini anakataa kufichua majina ya watu hao waliopanga njama hiyo ya mauaji ya Mboya, akitaja usiri uliogubika shughuli nyakati hizo kwani nchi ilikuwa imetoka kwa enzi za ukoloni.
Nyakati za utawala wa ukoloni shughuli nyingi zilikuwa zikiendeshwa kisiri na baada ya watu kulishwa kiapo.
“Unajua mau mau ilikuwa bado ni mwingi na hawa watu hawakutaka mambo yao yatoke nje. Kila kitu kilikuwa unalishwa kiapo,” anasema Ndwiga.
Anadai mpango huo wa kumuua Mboya ulipokamilishwa, alipewa pesa za kununua bastola tatu katika soko haramu karibu na mpaka wa Kenya na Somalia.
Ndwiga anasema kazi yake ilikuwa ni kutambua bunduki hizo, kuzilipia kisha kurejea kisiri jijini Nairobi. Mtu mwingine alipaswa kutekeleza kibarua cha kuzisafirisha hadi Nairobi.
Baadaye, watatu hao walipewa bunduki hizo.
Ndwiga hafichui jina la yule aliyepanga na kufadhili ununuzi na usafirishaji wa bunduki hizo hadi Nairobi.
Lakini anaeleza kuwa bastola hizo zilinunuliwa kutoka nje ya nchi ili kuzuia uwezekano wa kugunduliwa kuwa zilikuwa za serikali, wakati wa uchunguzi.
“Ukisikia mambo kama hayo ni plan ndefu. Si mtu moja anapanga ni kama revolution. Haiwezi pangwa na mtu mmoja.” Ndwiga anasema.
Kabla ya Mboya kuwasili nchini kutoka jijini Addis Ababa, Ethiopia, ambako alihudhuria mkutano wa mawaziri wa masuala ya Kiuchumi Afrika, watatu hao waliitwa mahala ambako walikuwa wakikutana kila mara.
Kila mmoja wao alikabidhiwa bastola na kupewa maagizo ya kumfuata na kumuua waziri huyo.
Walijulishwa kwamba Mboya angekuwa katikati mwa jiji kwa mkutano na maafisa wawakilisha wa wafanyakazi kwa sababu alikuwa kiongozi wa wafanyakazi.
Walikutana katika mkahawa mmoja karibu na kituo cha magari ya uchukuzi cha Tea Room kupanga mikakati ya jinsi ya kumkabili Mboya.
Siku ya tukio, Ndwiga anadai nafsi yake ilimwambia asimsaliti Mboya. Alitafakari jinsi ya kujiondoa kwenye mipango hiyo ya mauaji.
Mzee huyo anasema aliamua kukaa nyuma ya wenzake wawili wakielekea barabara ya Moi ambako Mboya alitembelea duka la dawa.
Ndwiga anadai alijitoma ndani ya gari la uchukuzi wa abiria na kuelekea nyumbani kwake Embu.
Tulipomuuliza mbona alijiondoa ilhali alishiriki mipango hiyo, alisema nafsi yake ilimwambia asiwaamini wenzake wawili kwani yeye ndiye alikuwa mtu kutoka jamii tofauti ya Embu. Wenzake walitoka jamii ya Agikuyu.
Ni wakati huo ambapo kundi la viongozi kutoka Kiambu na waliokuwa na ushawishi mkubwa serikalini walitangaza kuwa mamlaka ya urais haungewahi kuvuka mto Chania na kuelekea upande mwingine mwa Kenya.
Anasema kwa kwamba uzee ulikuwa umemwandama Rais Jomo Kenyatta, makamu wake wa Rais Jaramogi Oginga Odinga alikuwa amefukuzwa Kanu na Joseph Murumbi aliyejaza nafasi ya Odinga pia aliondolewa, Mboya ndiye alikuwa tisho kubwa.
Kundi hilo maarufu kama “Kiambu Mafia” lilifanikisha uteuzi wa Daniel Arap Moi kuwa Makamu wa Rais.
Hii ni kwa sababu kundi hilo lilidhani Moi hakuwa na ushawishi mkubwa.