Jinsi vuguvugu la vijana Kenya Moja linaweza kuharibia hesabu Ruto, Raila na Gachagua
MRENGO mpya wa Kenya Moja unaosukwa na wanasiasa waliojitenga na kambi za Rais William Ruto, Raila Odinga na aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua unatarajiwa kuharibu hesabu za kisiasa kwa kambi hizo katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Kenya Moja ilizinduliwa Jumapili na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna na Mbunge wa Githunguri Gathoni Wamuchomba aliyejitenga na kambi ya Bw Gachagua.
Wengine walio katika kambi hiyo mpya ni Mbunge wa Kabuchai Majimbo Kalasinga, Jack Wamboka (Bumula), Joshua Kimilu (Kaiti) na Mbunge wa Kitutu Masaba Clive Gisairo (ODM).
Bw Sifuna aliweka wazi kwamba katu hawezi kumuunga mkono Rais Ruto na yuko tayari kuondoka ODM ikiwa chama hicho kitamuunga mkono kiongozi wa taifa katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Bi Wamuchomba, ambaye amewahi kujihusisha na kambi kadhaa za kisiasa, anaonekana kupata makao mapya ya kisiasa katika Kenya Moja kama mwakilishi wa wanasiasa wa Mlima Kenya.
Huku ulingo wa siasa ukishamiri mijadala kuhusu iwapo Rais Ruto anafaa kuhudumu muhula mmoja au miwili, wapinzani wake wameibuka kuwa mwiba kwa Rais Ruto na Bw Gachagua, aliyetimuliwa afisini Oktoba mwaka jana.
Wachanganuzi wanaonya kuwa kuchipuka kwa muungano wa Kenya Moja kunaweza kuendeleza kauli mbiu ya mwaka jana kwamba Rais Ruto aondoke pamoja na Bw Gachagua.
Wengine pia wanasema Bw Odinga, ambaye ni mwandani wa Dkt Ruto, pia anapaswa kuondoka pamoja na yeye ili kutoa nafasi kwa mwamko mpya wa kisiasa.
Bw Gachagua amejiunga na kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka, kiongozi wa DAP-Kenya Eugene Wamalwa, aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i na Gavana wa Trans Nzoia George Natembeya.
Japo Kenya Moja inapinga utawala wa Ruto, haijaonyesha nia ya kujiunga na mrengo wa Gachagua na Musyoka. Hii ina maana kuwa imeunda mrengo mpya ndani ya Upinzani.
“Hali hii inakanganya na kuenda kinyume na mfumo wetu wa upigaji kura – uliojikita kwenye misingi ya kikabila na kimaeneo. Japo Kenya Moja inategemea kura za vijana, viongozi wake wanakaribia umri wa miaka 50,” anasema mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Festus Wangwe.
Anasema japo vijana wa Gen Z ni wenye umri wa kati ya miaka 16 na 28, viongozi wa muungano huo mpya wamezidi umri huo kwa umbali ni Sifuna ni mwenye umri wa miaka 43 na huku Wamuchomba akiwa na umri wa miaka 50.
Pili, japo Kenya Moja inamezea kura za Gen Z, tapo hilo la wapiga kura limechoshwa na mtindo wa zamani wa upigaji kura.
Kulingana na Billy Mwangi, mwanaharakati wa Gen Z na aliyetekwa nyara Embu, nia ya kuu ni mabadiliko wala si siasa za kutenga na kugawanya.
Babu Owino, Mbunge wa Embakasi Mashariki, 35, alipongeza ujio wa vuguvugu jingine la kisiasa lakini akaonya kuwa migawanyiko miongoni mwa wanasiasa wa upinzani, itafaidi mrengo tawala wa Dkt Ruto.