Habari za Kitaifa

Jowie ahukumiwa kifo kwa kumuua Monicah Kimani

March 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA RICHARD MUNGUTI

MSHTAKIWA Joseph ‘Jowie’ Irungu amehukumiwa kifo kwa kumuua mfanyabiashara Monicah Kimani.

Jaji Grace Nzioka mnamo Jumatano alisoma hukumu baada ya kutoa maelezo ya kina kuhusu kesi hiyo ya tangu Septemba 2018.

“Ninaondoa uwezekano wa kifungo cha nje kwa mshtakiwa na kusalia na ama kifungo cha jela kwa muda, jela maisha, au kifo,” akasema jaji Nzioka.

Aidha alieleza kwamba kifungo cha nje kingewezekana tu ikiwa mshtakiwa angekiri shtaka na kuieleza mahakama kwamba alikuwa tayari kubadilika kuwa mtu mzuri katika jamii.

Jaji Nzioka alisema ijapokuwa Mahakama ya Upeo iliharamisha adhabu ya kifo, haikuamuru itolewe katika vitabu vya sheria.

“Mahakama ya Upeo ilipoharamisha adhabu ya kifo, ilisema adhabu iwe ikitolewa katika visa vya kipekee kama hiki cha Monicah aliyeuawa kinyama hata bila ya kumuudhi Jowie,” alisema.

Jaji huyo alisema mauaji ya kinyama ya wanawake yamekithiri huku akinukuu ripoti ya Umoja wa Mataifa (UN) kwamba “katika kila siku mbili mwanamke huuawa humu nchini.”

Alisema ripoti ya kutetea haki za binadamu nchini ilisema “wanawake 500 waliuawa kati ya 2016 na 2024”.

Pia alinukuu ripoti iliyochapishwa na gazeti la Daily Nation kwamba wanawake 16 waliuawa Januari 2024.

“Jamii inatarajia mahakama ziwachukulie hatua kali na kupitisha adhabu kali dhidi ya wanaowaua wanawake,” Jaji Nzioka alisema.

Pia alimnukuu Dkt Johansen Oduor aliyefanyia upasuaji maiti ya Rita Mueni, mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Jomo Kenyatta (JKUAT) aliyekatwa kichwa na mwili wake ukakatwakatwa vipande na kutupwa ndani ya pipa la taka.

Alisema Dkt Owuour alisema “hiki ndicho kisa cha kwanza katika taaluma yangu ya upasuaji maiti nilichoshuhudia kilikuwa cha kusikitisha na kuhuzunisha”.

Jaji huyo alisema lazima sheria ichukue mkondo wake na adhabu kali kutolewa dhidi ya wahusika.

Jaji huyo alisema Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) kupitia kiongozi wa mashtaka Bi Gikui Gichuhi , familia ya Monicah na majirani wao waliomba mshtakiwa akabidhiwe adhabu kali ya kunyongwa.

Bi Gichuhi katika mawasilisho yake alisema Jowie alimuua Monicah kwa njia ya kinyama kabisa.

Alimfunga kwa Kamba mikono na miguu kisha akamchinja kwa kisu cha kijeshi.

Jowie alikuwa amepanga kumuua Monicah, kwa vile aliiba kitambulisho cha Kibarua katika makazi ya Royal Park Estate Lang’ata alichotumia kuingia katika lango la Lamuria Gardens , Kilimani.

Pia alikuwa amevalia Kanzu ya Kiislamu na baada ya kutekeleza mauaji hayo ya kinyama, aliichoma.

Hatimaye alitoa habari za uwongo kwa polisi kwamba alishambuliwa na majambazi katika lango la Royal Park.

Jaji alisema Jowie ni mtu wa hasira kali kiasi kwamba alikuwa akiwatisha mabawabu katika makazi ya Monicah na pia ya aliyekuwa mpenziwe Jacque Maribe ambaye aliachiliwa huru katika kesi hiyo.

Lakini Jaji Nzioka alimwamuru DPP amfungulie Bi Maribe mashtaka ya kutoa habari za uongo kwa polisi kwamba “Jowie alishambuliwa na majambazi ilhali ndiye alijipiga risasi ndani ya nyumba yao Royal Park.”

Mshtakiwa ana haki ya kukata rufaa.

Soma Pia: Kinaya nduguye Monicah kumtaka Jowie kupasha wanahabari mauaji aliyotekeleza