Habari za Kitaifa

Jumatatu, Machi 31, 2025 ni holidei, Waziri Murkomen atangaza

Na CHARLES WASONGA March 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imetangaza Jumatatu, Machi 31, 2025 kuwa siku ya mapumziko kote nchini.

Kupitia Gazeti Rasmi la Serikali toleo la Ijumaa, Machi 28, 2025, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen alitangaza kuwa siku hiyo imetengwe kwa ajili ya sherehe za sikukuu ya Idd-ul-Fitr.

“Umma unajulishwa kwamba, kwa mujibu wa mamlaka yanayotokana na sehemu ya 2 (1) ya Sheria kuhusu Siku Kuu, Waziri wa Usalama wa Ndani na Usimamizi wa Kitaifa anatawaza Jumatatu, Machi 31, 2025 kama siku ya mapumziko kwa maadhimisho ya Idd-ul-Fitr,” Bw Murkomen akaeleza.

Sikukuu ya Idd-ul-Fitr husherehekewa na Jamii ya Waislamu kote ulimwenguni kwa sababu huashiria mwisho wa mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan.

Ni mojawapo ya sikukuu mbili zinazosherehekewa na Waislamu na huadhimishwa katika siku tatu za kwanza za Shawwal, ambayo ni mwezi wa 10 katika Kalenda ya Uislamu.

Waislamu kote ulimwenguni wamekuwa wakizingatia mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, mojawapo ya nguzo tano za dini hiyo.