Habari za Kitaifa

Kadhi Mkuu atangaza rasmi mwisho wa Mfungo wa Ramadhani

April 9th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA WACHIRA MWANGI

Kadhi Mkuu Abdulhalim Hussein ametangaza mwisho wa Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani Jumanne baada ya kuonekana kwa mwezi mpya maeneo ya Mombasa, Lamu, Garsen na Mandera.

Kadhi huyo sasa amesema rasmi kwamba sherehe ya Idd-Ul-Fitr itafanyika Jumatano, alivyokuwa ametangaza Waziri wa Usalama Kithure Kindiki.

Kadhi Mkuu Abdulhalim Hussein akizungumza na simu ambapo alitangaza kuonekana kwa mwezi maeneo ya Mombasa, Lamu, Mandera na Garsen. Picha|Wachira Mwangi

“Tunamshukuru Mungu kwa neema na baraka zake. Ametuwezesha kufunga, kusali wakati wa Mwezi Mtukufu,” akasema Bw Hussein.

Alisema waumini walishiriki kwenye shughuli mbali mbali za kusaidia maskini, kukariri Kurani na mashindano mengine.

“Tunamuomba Mungu akubali funga zetu na matendo yetu mazuri na kutupatia fursa ya kufanya mengine mazuri siku za usoni.”

Alitaja sherehe za Idd kuwa siku za furaha na wakati wa kutoa shukrani na kusherehekea na wengine.

Ameomba waliojaaliwa mali nyingi kugawia wasio na chochote kwenye jamii.

Ameshukuru pia serikali za kaunti na ya kitaifa kwa usalama wa hali ya juu wakati wa mwezi wa Ramadhani.