Kahariri, Haji waonya watu wanaoendeleza ‘uchochezi’ wa “Ruto must go”
WAKUU wa usalama wameonya dhidi ya njama zozote za kupindua serikali kwa njia zisizo za kikatiba, wakati ambao kauli ‘Lazima Ruto Aende’ imekuwa maarufu katika mikusanyiko ya umma kama ishara ya kutoridhishwa na utawala wa Rais William Ruto.
Mkuu wa Majeshi (CDF) Jenerali Charles Kahariri na Mkurugenzi Mkuu wa Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS) Noordin Haji, Alhamisi, Machi 27, 2025 walisisitiza kuwa mabadiliko yoyote ya uongozi lazima yafanyike kwa mujibu wa Katiba.
Akizungumza katika Chuo cha Kitaifa cha Ujasusi na Utafiti (NIRU) jijini Nairobi wakati wa mhadhara wa kwanza uliohutubiwa na Bw Haji, Jenerali Kahariri alisisitiza kuwa Wakenya hawapaswi kuruhusu hali ya machafuko kutawala nchini humu.
“Hata watu wanapotekeleza haki zao, ni lazima tuwe ndani ya mipaka ili tusiingize nchi katika vurugu. Kama jeshi, msingi wetu ni kwamba hatuhusiki na siasa. Hatumuungi mkono mwanasiasa yeyote, bali tunalinda Katiba na serikali iliyopo madarakani,” alisema Bw Kahariri.
Aliendelea: “Kwa hivyo, watu wengine wanaposema wamechoshwa na serikali hii, serikali waliyochagua wenyewe, na kusema ‘lazima iondoke,’ hiyo ‘lazima iondoke’ inapaswa kufanywa kwa mujibu wa Katiba.”
Kauli yake inajiri wakati ambapo joto la kisiasa limepanda huku umati wa watu katika mikutano mbalimbali ukionekana kutumia kauli ya ‘Lazima Ruto Aende!’ kama njia ya kushinikiza kuondolewa kwa Rais madarakani.
Kauli hii imesikika katika vilabu mbalimbali vya burudani nchini na pia wakati wa mechi kati ya Harambee Stars na Gabon katika uwanja wa Nyayo, ambapo Rais Ruto na kiongozi wa ODM, Raila Odinga – ambao sasa wamefikia makubaliano ya kushirikiana – walihudhuria.
Alhamisi, Jenerali Kahariri pia alizungumzia madai ya jeshi kuhusika katika kukabiliana na waandamanaji, akisisitiza kuwa wanajeshi wa KDF hawashiriki siasa lakini wana jukumu la kulinda taifa.
“Kwa hivyo, kwa wale wanaouliza kwa nini jeshi linatumwa, tuna wajibu wa kulinda Katiba na taifa,” alisema.
Waziri wa Ulinzi, Soipan Tuya, wiki iliyopita pia aliambia Seneti kuwa ‘ingawa jukumu la msingi la usalama wa ndani linahusu mashirika mengine maalumu kama Huduma ya Polisi wa Kitaifa (NPS) na Huduma ya Kitaifa ya Ujasusi (NIS), KDF inaweza kutumwa iwapo kutatokea tishio la ndani dhidi ya mipaka ya Kenya na uhuru wake’.
Alisema kuwa kutumwa kwa KDF Juni 25, 2024, wakati bunge lilipovamiwa na waandamanaji wa Gen-Z, kulinuiwa kusaidia NPS, kama vile majukumu mengine ya KDF ya kusaidia taasisi nyingine za serikali.
Kwa upande wake, Bw Haji alionya dhidi ya siasa za mgawanyiko na akatoa wito kwa umma kuepuka chuki za kisiasa.
“Siasa za mgawanyiko zimepata uwanja mpya mitandaoni. Hili linagawanya watu wetu na kudhoofisha mshikamano wa kitaifa, ilhali mshikamano wa kitaifa unaendana na usalama wa kitaifa na maslahi ya taifa,” alisema.
Alionya kuwa ushindani wa kisiasa usipodhibitiwa, unaweza kusababisha hali ya kutokuwa na utulivu ambao unaweza kuchochea hasira za umma.
Bw Haji aliwataka Wakenya kuwa na mshikamano na kuonya kuwa “silaha ya ukabila inaleta mgawanyiko na kuathiri jamii, hivyo kuhatarisha umoja na uthabiti wa kisiasa wa Kenya”.
Mgawanyiko wa kikabila, alisema, ni hatari kwa taifa kwani huchochea migogoro inayorudisha nyuma maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Mhadhara huo uliwaleta pamoja wakuu wa usalama, viongozi wa kidini, Chama cha Mawakili Kenya (LSK), mashirika ya kijamii, vyombo vya habari, wawakilishi wa Bunge la Mwananchi na waendeshaji wa bodaboda.
Rais wa LSK, Faith Odhiambo, aliwataka maafisa wa usalama kutojihusisha na siasa.
“Swali la mauaji ya kiholela na matumizi mabaya ya polisi linapaswa kushughulikiwa kupitia Mamlaka Huru ya Uangalizi wa Polisi (IPOA). Hata hivyo, utendaji wake bado unatia wasiwasi,” alisema.