Habari za Kitaifa

Kama sio Raila, serikali yangu ingeporomoka, afichua Ruto

Na NDUBI MOTURI, BENSON MATHEKA October 18th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Rais William Ruto, jana alitoa ushuhuda wa kipekee na wa kugusa moyo kuhusu mchango mkubwa wa Raila Odinga katika kuokoa taifa wakati wa maandamano makubwa ya vijana wa kizazi cha Gen Z mnamo mwaka 2024.

Akihutubia taifa wakati wa ibada ya kitaifa ya wafu ya Waziri Mkuu huyo wa zamani katika Uwanja wa Nyayo, Rais Ruto alikiri kwa mara ya kwanza hadharani kwamba serikali yake ilinusurika kuporomoka kwa sababu ya  usaidizi wa Raila Odinga ambaye alikuwa mpinzani wake wa muda mrefu.

“Tulikuwa tumeshirikiana awali katika Pentagon, tukaja kuwa wapinzani. Lakini mwaka jana, njia zetu zilikutana tena,  safari hii si kwa ushindani, bali kwa ajili ya kuokoa taifa,” alisema Ruto kwa hisia nzito.

Rais alirejelea miezi ya maandamano katikati ya mwaka 2024 ambapo maelfu ya vijana walimiminika barabarani wakipinga ufisadi, gharama ya juu ya maisha, na ukosefu wa uwajibikaji serikalini. Maandamano hayo yaliyopangwa  mitandaoni yalitikisa misingi ya utawala wa  Kenya Kwanza.

Katika hali  ambayo haibainika wakati huo, Raila alichukua nafasi ya mpatanishi kimya kimya, na akasaidia kuweka msingi wa serikali jumuishi. Rais mwenyewe alithibitisha hilo hadharani jana.

Kupitia ushawishi wa Raila, wafuasi wake waaminifu waliteuliwa kushikilia nyadhifa muhimu serikalini. John Mbadi aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha, Hassan Joho waziri wa madini, Opiyo Wandayi kuwa Waziri wa Kawi, Wycliffe Oparanya kuwa Waziri wa Ushirika, huku Beatrice Askul akiongoza Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais alisema hakuzungumza kama mshindi wa kisiasa, bali kama mtu aliyenusurika na kusaidiwa na mtu aliyekuwa mpinzani wake wa muda mrefu.

“Tulikuwa washirika na wapinzani, marafiki na mahasimu, lakini daima tulikuwa wazalendo,” alisema, akimkumbuka Raila kama “mpatanishi, mzalendo, na dira ya maadili.”

Akimtaja Raila kama “jasiri, mwenye nguvu thabiti na moyo usioyumba,” Rais Ruto alisisitiza kuwa “historia itamhukumu Raila kwa haki na kwa wema.”

Kwa sauti iliyojaa hisia, alihitimisha hotuba yake kwa kuimba ubeti wa wimbo wa Raila alioupenda — Jamaica Farewell, akisema:
“Kwa wimbo huu, tunakushukuru, Baba, kwa kila hatua uliyopiga kwa ajili yetu sote.”

Rais alitambua kuwa katika kujenga taifa, si lazima wote wakubaliane kisiasa, bali kila mmoja ana nafasi ya kuhudumu kwa manufaa ya Kenya.

Aidha, alisisitiza kuwa urithi wa Raila hautapimwa kwa vyeo alivyowahi kushikilia, bali kwa mchango wake kwa taifa: kupigania demokrasia, kushinikiza mageuzi ya katiba,na kusimama na wale waliotengwa na mfumo wa utawala.

“Katika kila changamoto tuliyokutana nayo, Raila alionyesha kwamba kuwa mpinzani wa serikali si kuwa adui wa nchi. Ni kuwa mlinzi wa misingi ya haki na maadili,” alisema Rais.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta alitoa heshima za kipekee kwa Raila Odinga akimtaja kama mzalendo wa kweli na mtu aliyefanikisha historia ya taifa.

“Raila aliipenda Kenya kuliko kitu kingine chochote. Alikuwa baba kwa wote, hakuwahi kuwa na ukabila, na aliwapenda Wakenya wote kwa usawa,” alisema Rais Kenyatta, akikumbuka jinsi nyumba ya Odinga ilivyokuwa wazi kwa watu wa matabaka na makabila yote.

Kauli hiyo haikuwa tu heshima ya kisiasa, bali pia ilikuwa kauli ya upatanisho binafsi kutoka kwa aliyekuwa mpinzani wake wa kisiasa kwa miaka mingi.

“Historia ya Kenya haiwezi kuandikwa bila jina la Raila Odinga kuwa miongoni mwa ya kwanza,” aliongeza. “Hadithi ya demokrasia, ugatuzi, na utetezi wa haki za wananchi wa kawaida  zote zina alama yake.”

Sauti ya Kenyatta ilibeba uzito wa mtu aliyeelewa gharama ya uhasama wa kisiasa, lakini pia nguvu ya maridhiano.

“Raila ametutoka kimwili, lakini katika mioyo yetu na katika roho ya taifa letu, ataendelea kuishi milele,” alisema kwa sauti ya huzuni.