Kambi mpya za ‘kukutana na Yesu’ Kilifi zachunguzwa
MAAFISA wa upelelezi wanaochunguza vifo vinavyohusishwa na kundi la kidini eneo la Kwa Binzaro huko Kilifi, wameanza msako kuhusu maeneo ya siri ya kuwazuia waathiriwa mjini Malindi, ambako inadaiwa wanafichwa kabla ya kupelekwa msituni kwa mfungo hatari kwa lengo la “kukutana na Yesu.”
Wachunguzi wanaamini kuwa maeneo hayo ya siri si ya kuwazuilia pekee, bali ni vituo vya kufundisha itikadi kali, ambapo waathiriwa hupotoshwa na kuingizwa katika mafundisho ya kufunga hadi kufa kabla ya kupelekwa msituni kuanza mfungo halisi.
Waendeshaji wa vituo hivyo vya siri wanadaiwa kuwa wafuasi wa mhubiri Paul Mackenzie na washirika wa kanisa lake la Good News International, waliotoroka wakati wa msako wa usalama mnamo 2023 baada ya kugunduliwa kwa makaburi ya halaiki katika msitu wa Shakahola, ambapo zaidi ya washukiwa 90 walikamatwa.
Wale waliokamatwa tayari wanakabiliwa na mashtaka mazito yakiwemo mauaji, kuua bila kukusudia, kufundisha itikadi kali, kuwatesa watoto, na kunyima watoto haki ya kupata elimu ya msingi.
“Maeneo haya ya siri yanatumiwa kama kambi za kupotosha. Taarifa zetu za kijasusi zinaonyesha watu wanazuiliwa humo, lakini changamoto kubwa ni kutambua maeneo hayo halisi,” alisema mpelelezi mmoja ambaye hakutaka kutajwa jina.
Kwa mujibu wa chanzo hicho cha polisi, kundi hilo pia linahusishwa na kukamatwa kwa watu 11 hivi majuzi kuhusiana na vifo vipya vya waathiriwa huko Kwa Binzaro.
Polisi wana hofu kuwa watoto zaidi ya kumi waliopotea huenda wamezikwa kwenye makaburi kijijini humo, na sita wanaripotiwa kutoka familia moja.
Wakazi waliozungumza na Taifa Leo walieleza kuwa oparesheni iliyopelekea kukamatwa kwa Mackenzie haikuwakamata wote waliokuwa washirika wa kanisa lake waliokuwa wakijihusika na kufunga na misimamo mikali ya kidini msituni.
“Tumekuwa na mashaka kwa muda mrefu kuhusu shughuli zisizoeleweka zinazofanyika kwenye msitu huo mkubwa. Tunaamini bado kuna watu waliotoroka mikono ya polisi na sasa wanaendelea na shughuli za kufundisha imani kali,” alisema Riziki Baya, mkazi wa Kwa Binzaro.
Mkazi mwingine alieleza kuwa eneo hilo huwa na shughuli nyingi kila mara, na harakati za watu kuingia na kutoka hufanya iwe vigumu kubaini nani anaondoka na nani anabaki msituni.
Waziri wa Usalama wa Ndani Kipchumba Murkomen alisema kuwa watu wenye nia mbaya wanatumia ukubwa wa ranchi ya Chakama, yenye takribani ekari 100,000, kujificha na kutekeleza uhalifu.Murkomen alikiri kuwa kupambana na misimamo mikali ya kidini si jambo rahisi, lakini akawahakikishia wananchi kuwa serikali inafanya kila iwezalo kukomesha tatizo hilo.
“Si kwamba tunaruhusu vitendo hivi haramu, lakini vita dhidi ya itikadi kali za kidini ni vigumu. Ni tatizo tata linalohitaji kushughulikiwa kwa makini,” alisema katika Jukwaa la Usalama huko Nakuru.
Serikali imefichua kuwa mtandao tata wa kufundisha itikadi kali unaohusiana na kundi hilo la kidini umeendelea kustawi licha ya juhudi za idara za salama.
Inadaiwa kuwa Mackenzie bado anawasiliana na baadhi ya wafuasi wake akiwa rumande, ambako anazuiliwa kuhusiana na vifo vya zaidi ya waumini 400 wa kanisa lake waliokufa kwa kufunga katika msitu wa Shakahola.
Kwa mujibu wa serikali, mfuasi mmoja aliyenusuriwa aliwaambia wachunguzi kuwa Mackenzie alimpigia simu kutoka gerezani.
“Tunataka kuelewa mazingira yaliyomfanya mtu huyu, ambaye tuliokoa kutoka msituni mwaka wa 2023, alirudi tena Kwa Binzaro,” alisema Bw Murkomen.
Mfuasi huyo, ambaye alikuwa amerejea kijijini kwao Kaunti ya Siaya baada ya kuokolewa kutoka Shakahola, alirudi tena na familia yake msituni kuendelea na mfungo huko Kwa Binzaro.
“Ukikutana na mtu anayesema anaenda kuomba juu ya Mlima Sinai kama Musa, utamzuia? Itikadi kali ni ngumu sana, lakini tunakabiliana nayo. Hatutaruhusu hali hii iendelee,” alisema Murkomen.
Idadi kubwa ya waliofariki Kwa Binzaro ni watoto, wengi wakihofiwa kuzikwa kwenye makaburi ya kina kifupi au kuachwa msituni kuliwa na wanyama wa porini.“Uhalifu huu sasa ni mauaji ya watoto wadogo ambao hawajui chochote kuhusu haya mafundisho,” alisema Murkomen.
Maafisa wa upelelezi wamepanua eneo la uchunguzi zaidi ya ekari tano walizokuwa wakichunguza awali Kwa Binzaro.Sasa wanafanya uchunguzi maeneo ya nje baada ya kugundua mifupa ya binadamu, vikiwemo vipande vya fuvu, katika maeneo ambayo awali hayakushukiwa kuwa na makaburi.
Mnamo Julai, maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) walipata kibali kutoka mahakama ya Malindi kuruhusu ufukuaji wa miili kufanya uchunguzi wa DNA na sumu.
Hata hivyo, mipango ya kuanza kuchimba kaburi Alhamisi ilikwama baada ya Daktari Mkuu wa Uchunguzi wa Vifo Serikalini, Johansen Oduor, pamoja na wataalamu wa kuhifadhi miili, kushindwa kufika eneo hilo.