Kampuni ya familia ya Joho kulipwa Sh9 bilioni kupisha ujenzi wa uwanja wa Talanta
KAMPUNI inayohusishwa na familia ya Waziri wa Masuala ya Madini, Hassan Joho italipwa Sh9 bilioni ili kuacha azma yake ya kupata ardhi ya ekari 79 kwenye barabara ya Ngong Nairobi, ambapo serikali inajenga uwanja wa Michezo wa Talanta.
Uwanja huo unaojengwa karibu na Uwanja wa Maonyesho wa Jamhuri kando ya barabara ya Ngong, ni mojawapo ya ambavyo Kenya inalenga kutumia kuandaa mechi za Kombe la Mataifa ya Afrika (AfCON) mwaka wa 2027.
Uwanja huo upo kwenye ardhi ya thamani kubwa ambayo umiliki wake unazozaniwa na serikali na Telkom Kenya, shirika linalodhibitiwa na Serikali.
Kampuni ya Telkom ilidai kwamba ujenzi wa uwanja huo ulianza kabla ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kukamilisha kutwaa ardhi yenyewe.
Kampuni hiyo ambayo kwa sehemu inamilikiwa na Serikali, ilifika mahakamani Desemba 2021 ikitaka fidia ya Sh15 bilioni kupisha ujenzi wa uwanja huo katika ardhi hiyo, ikisema kuwa serikali ilikuwa ikiinyima haki yake ya kumiliki mali hiyo.
Serikali inamiliki 40 kwa kila senti ya hisa katika telco, na inashiriki kikamilifu katika usimamizi wa kampuni.
Jaribio la utawala wa Rais wa zamani Uhuru Kenyatta kununua hisa za kibinafsi za asilimia 60 za kampuni hiyo lilibatilishwa na Rais William Ruto mwaka jana.
Madai ya Telkom ya kulipwa fidia ya ardhi ya uwanja wa Talanta yana uhusiano na Aftraco Limited, kampuni inayohusishwa na familia ya Waziri Joho.
Mnamo 2011 Aftraco ilikubali kununua shamba hilo kutoka kwa Telkom kwa Sh1.52 bilioni na kulipa Sh152 milioni, ikiwa ni asilimia 10 ya thamani ya ardhi hiyo.
Telkom, hata hivyo, iliacha kuuza ardhi hiyo kwa familia ya Joho. Aftraco ilianzishwa Agosti 4, 2009. Rekodi za usajili (BRS) zinaonyesha kuwa Aftraco inamilikiwa na Salim Sadru (hisa 500), Jane Jepkemboi Sumbeiywo (hisa 499) na wakili Hellen Alice Olwanda (hisa moja).
Anwani ya posta Bw Salim aliyotangaza kuwa yake katika ufichuzi wa BRS kwa Aftraco pia inatumiwa na Portside Freight Terminals.
Abubaker Ali Joho ana hisa 75 za Portside, huku Hussein Hamid Khamis ana hisa 25.
Bw Abubaker na Bw Salim pia ni wanahisa na wakurugenzi wa Autoports Freight Terminals Ltd, kampuni nyingine inayomilikiwa na familia ya Joho.
Kila moja yao ina hisa 250 katika Autoports.
Khamis Hamid pia ni mmiliki Autoports ikiwa na hisa 500. Autoports ilianzishwa Julai 5, 2012.
Hati za Huduma ya Usajili wa Biashara zinaonyesha kuwa kufikia 2023, kampuni hiyo ilikuwa imepata mkopo wa $16.125 milioni (Sh2.084 bilioni) kwa kufadhili shughuli zake.
IMETAFSIRIWA NA BENSON MATHEKA