Kashfa nyingine? Maswali yaibuka watahiniwa wakipata matokeo tofauti nyakati tofauti
NA WAANDISHI WETU
Hali ya sintofahamu imewakumba wazazi pamoja na wanafunzi wa shule mbalimbali baada ya kupata matokeo tofauti kupitia tovuti ya Knec.
Baada ya kutangaza matokeo ya mtihani Jumatatu, Januari 8, 2024 mwendo wa saa nne asubuhi, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu aliwaelekeza wazazi kupata matokeo kamili kwenye tovuti ya baraza la mtihani Knec.
Na hapo wanafunzi wengi walifaulu kupata matokeo asubuhi licha ya tovuti hiyo kugoma baadaye kutokana na msongamano mkubwa wa waliokuwa wanautembelea.
Soma kuhusu mtandao wa Knec ulivyogoma awali majira ya saa tano asubuhi.
Lakini kufikia jioni, imebainika kwamba matokeo hayo yamebadilika jioni ya Jumatatu.
Mtahiniwa mmoja wa Kenya High ambaye tunabana jina lake kwa sababu za kisheria, alipata alama ya A- alipoangalia matokeo na mzazi wake asubuhi. Lakini walipoangalia tena baadaye jioni walipata kwamba hali imebadilika kabisa na kwamba alama iliyojitokeza kwenye tovuti ni B+. Masomo yaliyoonekana kubadilishwa alama ni Kiswahili na Hesabu, ambapo wakati asubuhi yalionyesha alipata B+ na A- mtawalia, kufikia jioni ilionyesha amepata B- na B plain mtawalia.
Katika kisa kingine katika Nairobi School, mtahiniwa amekumbwa na hali hiyo hiyo. Asubuhi alipoangalia, alikuta alama yake ni B plain. Lakini alipoangalia baadaye akakuta amenyolewa alama hadi akaachwa na B-. Yeye vilevile amepata dosari hizo kwenye masomo ya Kiswahili na Hesabu, ambapo wakati awali alikuta amepata A- na C+ mtawalia, baadaye aliona amepunguziwa hadi B plain na C plain.
Ni hali iliyoibua maswali na wasiwasi miongoni mwa watahiniwa, wazazi na wadau kwa jumla, isijulikane kilichokuwa kinasababisha mabadiliko hayo ambayo si ya kawaida.
Kulingana na mdokezi katika shule ya Kenya High ambaye hakutaka kutajwa jina kwa sababu hana idhini ya kuzungumza na vyombo vya habari, wanaendelea kufuatilia tukio hilo kutoka wizara ya Elimu huku wakitarajia kwamba alama za awali zitadumishwa.
Aidha, wakati huo huo, shule hiyo imerekodi kuimarika kwa matokeo yake kwa kujipatia A 36, A- 118, B+ 106, B 65, B- 42.
Endelea kutegea hapa tukupashe yanayojiri…