Katibu matatani kwa kukaidi amri ya kulipa wanajeshi
MAHAKAMA Kuu imemwaagiza Katibu katika Wizara ya Ulinzi Patrick Mariru ajitetee kwa kukiuka amri ya kuwalipa wanajeshi 10 wa zamani Sh68.8 milioni la sivyo aadhibiwe kwa kufungwa gerezani.
Wanajeshi hao walizuiliwa na kuteswa mnamo 1982 baada ya jaribio la mapinduzi kutibuliwa na wanajeshi wa serikali waaminifu kwa utawala wa KANU.
Mahakamani imebainika kuwa Wizara ya Ulinzi inakumbwa na uhaba mkubwa wa fedha kwa kuwa ina deni la zaidi ya Sh4 bilioni linalodaiwa na wawasilishaji bidhaa ambao pia wamewasilisha kesi mahakamani.
Bw Mariru ameamrishwa afike mbele ya Jaji John Chigiti hapo Juni 23, 2025 saa tano mchana ili kueleza kwa nini hafai kuadhibiwa kwa kukaidi mahakama.
Alikiuka amri hiyo iliyotolewa miaka mitano iliyopita, Julai 25, 2018 iliyotaka wanajeshi hao walipwe kwa kupitishwa kwenye madhila makali.
Mahakama ilitoa uamuzi wa kuwalipa wanajeshi hao wa zamani mnamo Februari 15, 2012.
Jaji Chigiti alikataa maelezo ya katibu huyo kuwa kutolipwa kwa wanajeshi hao kunatokana na mbinu ambayo serikali imekumbatia ya kupunguza matumizi ya pesa.
kwenye wizara mbalimbali.
“Mahakama inatambua kuwa malipo ya wizara za serikali na mashirika hutegemea bajeti ambayo huidhinishwa na Bunge la Kitaifa. Hata hivyo, haifai kwa uamuzi uliotolewa zaidi ya miaka saba ukose kutimzwa ilhali shughuli za wizara zinaendelea,” akasema Bw Chigiti.
Haya yanakuja mwezi moja baada ya Jaji kutoa amri nyingine kwa katibu huyo kwenye kesi nyingine inayohusu kundi la wanajeshi 10 wa zamani.
Wanajeshi hao hawajalipwa Sh134 milioni kama fidia kutokana na kuvunjwa kwa haki zao baada ya mapinduzi hayo.
Makundi hayo mawili ya jeshi yalikuwa yakiwajibika chini ya jeshi la wanahewa na walifurushwa kazini baada ya mapinduzi dhidi ya serikali kufeli.
“Wizara haijapinga kiasi ambacho wanajeshi hao wanastahili kulipwa ila kijisababu hiki kuwa hawana pesa hakina mashiko,” akaongeza Bw Chigiti.
Wanajeshi hao mwanzoni walitunukiwa Sh23.5 milioni lakini kiwango hicho kimepanda hadi Sh68.8 milioni kutokana na faida na gharama nyingine.