Habari za Kitaifa

KDF: Tatizo kwenye injini ya helikopta ndilo lilimuua Jenerali Francis Ogolla

Na ELVIS ONDIEKI NA CECIL ODONGO April 12th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HELIKOPTA ambayo ilimuua Mkuu wa Majeshi Jenerali Francis Ogolla na wengine 11 mnamo April 18, ilianguka kutokana na kasoro kwenye injini yake, Ripoti ya Wizara ya Ulinzi imesema.

Jopo la uchunguzi liliangazia masuala sita ambayo yangesababisha ajali hiyo na likafikia kuwa tatizo la injini ndilo lilifanya helikpota hiyo ianguke.

Kwa mujibu wa jopo hilo, kabla ndege hiyo ianguke, kulikuwa na milio na kutokana na uchunguzi wao, hilo lilisababishwa na joto ndani ya injini. Ni joto hilo ndilo lilisababisha kuzima kwa injini.

“Mashahidi waliokuwa katika eneo ambalo ndege ilianguka, walisema walisikia milio hatari kutoka kwenye injini na hilo lilisababisha injini ya helikopta kuzima,” ikasema ripoti hiyo iliyotolewa Ijumaa, Aprili 11, 2025.

“Kutokana na ushahidi ambao ulikusanywa na kuthibitishwa, jopo la uchunguzi limeafikia kuwa helikopta KAF 1501 ilianguka kutokana na tatizo kwenye injini yake iliyosababisha injini kuzima,” ikaongeza.

Jopo hilo kwenye ripoti yake lilisema kuwa kutokana na hilo, Jeshi la angani limetathmini na kuangazia upya jinsi ndege zake zinavyotumika na zitahakikisha ziko hali sawa ili kuzuia ajali kama hiyo siku za baadaye.

Ndege iliyobeba Jenerali Francis Ogolla ilianguka saa nane na dakika 20 mnamo Aprili 18, 2024 katika kijiji cha Sindar, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.

Alikuwa amesafiri na watu 11 ambao walikuwa wanajeshi na walikuwa wakihudumu kwenye idara mbalimbali za ulinzi.

Wengine ambao walikuwa kwenye ndege hiyo ni Brigadier Swale Saidi (Kamanda aliyehusika na uhandisi na ufundi), Kanali Kasaine Ole Kuruta (mfanyakazi katika makao makuu ya jeshi ambaye alinusurika ajali hiyo) na Duncan Keitany (msimamizi kitengo cha oparesheni kwenye makao makuu ya jeshi).

Luteni Kanali David Sawe (Afisa anayehudumu katika kitengo cha miundomingi makao makuu ya jeshi), Meja George Benson Magondu (rubani) na Sora Mohamed (rubani mwenza) pia walikuwa kwenye helikopta hiyo.

Wengine ni Kapteni Hillary Litali (mlinzi na msaidizi wa Jenerali Ogolla), Sajini John Kinyua Mureithi (msimamizi wa kitengo cha ufundi kwenye ndege), Sajini Cliphonce Omondi (mlinzi wa Jenerali Ogolla).

Kwenye ndege hiyo, pia, walikuwepo Rose Nyawira ambaye alitoka kitengo cha mawasiliano cha Jenerali Ogolla sawa na Kapteni Frankford Karanja Mogire ambaye alinusurika mauti hayo.

Manusura wawili waliohojiwa walikuwa sehemu ya uchunguzi ulioafikia ripoti hiyo.

Walihojiwa na wanachama wa jopo la uchunguzi pamoja na mashahidi wengine 12.

Kabla ya mauti Ogalla, 62, alikuwa amezuru Chesitet, Kaunti ya Baringo ambako alifahamishwa kuhusu hali ya usalama eneo hilo kisha akaelekea makao ya jeshi ya Kainuk Kaunti ya Turkana ambako alizungumza na wanajeshi.

Baada ya hapo msafara wake ulielekea Chesegon, Pokot Magharibi ambako alizindua mradi wa kukarabati miundomsingi katika Shule ya Wavulana Cheptulel.

Mradi huo ulikuwa ukifadhiliwa na jeshi kama sehemu ya kuimarisha vita dhidi ya ujangili.

Baada ya kuondoka Chesegon akielekea Chuo cha Mafunzo ya Makurutu Kaunti ya Uasin Gishu ambako alikuwa akague ujenzi wa miundomsingi uliokuwa ukiendelea, ndipo helikopta hiyo ilianguka.

Mnamo Mei mwaka jana, 2024, wakati ambapo jopo hilo lilikuwa likiendelea na uchunguzi wake, viongozi wa Azimio walilipinga na kusema uchunguzi huo ungefanywa na kamati teule ya bunge.

Pia, viongozi wa Azimio walipendekeza wataalamu huru wa kimataifa wapokezwe jukumu la kuendesha uchunguzi wa jinsi helikopta hiyo ilivyoanguka na kusababisha mauti ya Jenerali Ogolla na wenzake.

Upinzani ulisema jeshi la wanahewa ni asasi ya kisiri ambayo shughuli zake haziko wazi kwa umma kwa hivyo, haliafiki mantiki ya uchunguzi huru, wenye uwazi na unaoaminika.

Kiongozi wa Wiper, Bw Kalonzo Musyoka ambaye alisoma taarifa ya upinzani wakati huo alidai huenda mauti ya Jenerali Ogolla yalihusishwa na siasa

Hii ni kutokana na madai ambayo hayakuthibitishwa kuwa alikuwa kati ya waliojaribu kubatilisha ushindi wa Rais William Ruto mnamo 2022.