Kibet Bull asema atapunguza matumizi ya mitandao ya kijamii baada ya kuachiliwa huru
MCHORAJI vibonzo Gideon Kibet, almaarufu Kibet Bull aliyeachiliwa huru Jumatatu baada ya kutekwa nyara jijini Nairobi mwezi jana alisema atapunguza shughuli zake katika mitandao ya kijamii.
Akizungumza baada ya kuachiliwa, Kibet alisema alikuwa buheri wa afya japo alitupwa eneo ambalo hakulifahamu na waliomteka, usiku wa kuamkia Jumatatu.
“Nitapunguza kidogo shughuli za mtandaoni kuendelea mbele,” alisema na kukataa kusimulia masaibu yake mikononi mwa waliomteka nyara.
Kibet alitangaza kuachiliwa kwake kupitia anwani yake ya mtandao wa X saa kadhaa baada ya vijana wengine wanne akiwemo kaka yake Ronny Kiplangat kuachiliwa huru akisema alitupwa eneo la Luanda, Kaunti ya Vihiga, kati ya saa tisa na saa kumi alfajiri siku ya Jumatatu.
Dadake Kibet, Bi Mercy Chelangat, awali alithibitishia Taifa Leo kwamba kakake aliwafahamisha kuwa yuko salama na kwamba alipata simu aliyoitumia kuchapisha kwenye akaunti yake ya X kwamba sasa alikuwa huru kutoka kwa watekaji wake.
“Tumezungumza naye na yuko salama kabisa. Alianza safari yake kurudi nyumbani na sasa yuko Nakuru ambako atalala usiku huu kabla ya kujiunga nasi nyumbani (Molo) kesho. Tuna furaha kubwa kwamba yuko hai. Leo ni siku ya furaha kubwa,” alisema Bi Chelangat.
Kuachiliwa kwake kulifikisha watano idadi ya watu ambao waliachwa sehemu tofauti za nchi, jambo ambalo limezua maswali kuhusu matukio ya utekaji nyara yanayoendelea.
Mchoraji huyo anayefahamika na wengi kutokana na uchoraji wake wa vibonzo vya Rais William Ruto alisema alishukuru Mungu kwa kuwa hai.
Kibet alitekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa usalama mnamo Desemba 24, 2024, muda mfupi baada ya kukutana na Seneta wa Busia, Okiya Omtatah, katika ofisi yake jijini Nairobi.