Habari za Kitaifa

Kilio cha haki mfadhili akipachika mimba mwanafunzi na mtoto kuuawa

Na MERCY KOSKEI April 6th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BINTI yake alipofaulu Mtihani wa Kitaifa wa Darasa la Nane (KCPE) mwaka 2023, Rehema* alihofia kuwa ndoto ya mtoto wake ya kujiunga na shule ya upili ingesalia kuwa ndoto tu, kutokana na ukosefu wa karo.

Hata hivyo, matumaini yalionekana pale rafiki wake wa karibu kanisani alipomjulisha kuhusu “Msamaria Mwema” aliyekuwa tayari kumfadhili mwanawe kikamilifu: kuanzia karo, sare za shule, hadi mahitaji mengine.

Kwa mujibu wa Rehema, mwanamke huyo alidai kuwa mfadhili huyo alikuwa amemfadhili mtoto wake ambaye alikuwa tayari amemaliza KCSE, na hivyo alitaka asaidie mtoto wa Rehema.

Akiwa mama wa kipato cha chini anayeishi Salgaa, Kaunti ya Nakuru, Rehema alikubali bila kusita, na kweli mfadhili huyo alilipa karo ya mwaka mzima wa bintiye.

“Tulikuwa na uhusiano wa karibu kanisani. Nilidhani ameguswa na hali yangu. Walitoa kila kitu – binti yangu hakukosa chochote mwaka mzima,” Rehema alisema kwa furaha wakati huo.

Lakini hakujua kwamba kulikuwa na nia fiche nyuma ya ukarimu huo.

Mwanaume aliyekuwa akilipa karo alitumia nafasi hiyo kumdhulumu kimapenzi msichana huyo wa miaka 17 na hatimaye akamsababishia ujauzito.

Baada ya kugundua ukweli huo, Rehema alimwita mwanamke huyo nyumbani kwake kumhoji, lakini alijibu kwa vitisho, akidai kwamba mwanaume aliyempa ujauzito binti yake ni mtu mwenye ushawishi mkubwa na angeweza kutumia pesa kuzuia haki.

“Mwanamume huyo ni mzee anayeheshimika kanisani kwetu. Sina uwezo wa kupambana naye. Nilinyamaza na kumuachia Mungu,” alisema Rehema kwa uchungu.

Mnamo Aprili 1, msichana huyo alianza kupata uchungu wa uzazi na akakimbizwa katika Hospitali ya Rongai kabla ya kuhamishiwa Hospitali ya Mafunzo na Rufaa ya Nakuru. Hata hivyo, mwanamke huyo alishauri apelekwe katika hospitali ya kibinafsi ndani ya Rongai ambako alijifungua mtoto wa kiume.

Siku chache baadaye, msichana huyo aliruhusiwa kutoka hospitali na kurejea nyumbani akiwa na mama yake na mwanamke huyo. Mambo yalibadilika ghafla.

Mwanamke huyo alimtumia Rehema Sh1,400 kupitia MPesa kununua mahitaji ya nyumbani. Wakati Rehema alipokuwa dukani, alipokea simu akielezwa kuwa mtoto alikuwa ameugua ghafla.

Aliporejea nyumbani, alimkuta mjukuu wake akitapika. Uchunguzi ulionyesha kuwa alikuwa amepatiwa sumu. Rehema alipata dawa ya kuua wadudu kwenye mfuko wa mwanamke huyo na kuikabidhi polisi. Mtoto alifariki dunia, na mwili wake ulipelekwa katika hifadhi ya maiti ya Hospitali ya Rufaa ya Nakuru.

Jirani na maafisa wa usalama walifika kwa haraka baada ya Rehema kumfungia mwanamke huyo ndani ya nyumba.

Msichana huyo aliambia Taifa Leo kuwa mwezi mmoja baada ya kujiunga na Kidato cha Kwanza, mwanamke huyo alimchukua kwa kisingizio cha kwenda kununua mahitaji ya shule. Wakiwa njiani, walikutana na mwanaume aliyekuwa anajulikana kama Macharia—mfadhili wake.

Walielekea Nakuru ambako waliingia kwenye chumba cha kulala. Hapo ndipo msichana huyo alibakwa kwa mara ya kwanza. Mwanaume huyo alimwambia asithubutu kueleza mtu yeyote na akifichua angeuawa.

Tukio hilo lilijirudia mara tatu. Kila mara, msichana alipewa pesa kama ‘shukrani’ na mwanamke huyo alimtuliza kuwa mambo yote yako sawa.

“Wakati nilipomweleza kuwa nilipata mimba, alisema atanisaidia kwa kila kitu. Nilikuwa naogopa kusema ukweli,” alisimulia.

Mnamo Ijumaa, Afisa wa Upelelezi wa Jinai wa Kaunti Ndogo ya Rongai, Donnata Otieno, alithibitisha kuwa mshukiwa, Jennifer Makomore, alifikishwa Mahakama ya Molo na akazuiliwa kwa siku14 polisi wakakamilishe uchunguzi wao.