Kindiki avishwa taji la Naibu Kiongozi wa UDA, akabidhiwa manifesto
NAIBU Rais Kithure Kindiki amekabidhiwa rasmi wadhifa wa Naibu Kiongozi wa Chama cha United Democratic Alliance (UDA) kuchukua nafasi ya mtangulizi wake Rigathi Gachagua.
Kwenye taarifa Jumanne, Novemba 11, Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) la chama hicho limesema wamechukua uamuzi huo kwa sababu kulingana na vipengele vya 75 (3) na 45 (7) Bw Gachagua hawezi kuendelea katika wadhifa huo wa “umma”.
“Baada ya kuondolewa mamlakani na Bunge la Kitaifa na hatua hiyo kuidhinishwa na Seneti na kuhusiana na mahitaji ya vipengele vya 75 (3) na 45 (7) vy Katiba, Rigathi Gachagua hawezi kuendelea kutekeleza majukumu ya naibu kiongozi wa chama na hivyo anakoma kushikilia cheo hicho,” taarifa hiyo ikasema.
“Kwa hivyo, Baraza Kuu la Kitaifa la UDA limeamua kumtaja Profesa Kithure Kindiki kuwa Naibu Kiongozi, kuanzia sasa,” ikaongeza.
Hata hivyo, taarifa hiyo haikubaini ikiwa Bw Gachagua amefurushwa chamani au la.
Majuma mawili yaliyopita Katibu Mkuu wa UDA Hassan Omar alidokeza kuwa baada ya Gachagua kuvuliwa wadhifa wa Naibu Kiongozi wa chama hicho atafurushwa kabisa kwa “sababu mienendo yake hailandani na sera na maadili ya UDA.”
Kulingana na Katiba ya chama hicho kinachoongozwa na Rais William Ruto, naibu rais ndio anapaswa kushikilia wadhifa wa Naibu Kiongozi.
Profesa Kindiki aliapishwa rasmi kuwa Naibu Rais wa tatu chini ya Katiba ya sasa katika hafla iliyofanyika katika uwanja wa KICC, Nairobi Novemba 1, 2024.