Kindiki kuanza rasmi kazi ya naibu rais akiidhinishwa na kuapishwa
PROFESA Kithure Kindiki aliyeteuliwa kuwa Naibu Rais wa tatu wa Kenya kuchukua nafasi ya Bw Rigathi Gachagua aliyeondolewa mamlakani na seneti Alhamisi usiku, Oktoba 17, 2024 ataanza kutekeleza majukumu baada ya kuidhinishwa na Bunge la Taifa na kuapishwa rasmi.
Rais William Ruto aliwasilisha jina la Prof Kindiki kwa Bunge la Kitaifa Jumatano asubuhi, Oktoba 18, saa chache baada ya spika wa seneti Amason Kingi kuchapisha kuondolewa kwa Bw Gachagua kama naibu rais.
Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetangula, katika kikao spesheli kilichofanyika Ijumaa (Oktoba 18), alitangaza kuwa alipokea mawasilisho kutoka kwa seneti kumfahamisha kuwa maseneta walikuwa wameidhinisha kutimuliwa kwa Bw Gachagua kwa kumpata na hatia ya mashtaka matano kati ya kumi na moja yaliyokuwa kwenye hoja ya kumuondoa mamlakani.
“Leo asubuhi, nimepokea barua kutoka kwa Rais, akiteua Profesa Kithure Kindiki kuwa naibu rais kufuatia kiti hicho kubaki wazi baada ya aliyekishikilia kuondolewa Alhamisi usiku,” Spika Wetangula aliambia wabunge.
Katika notisi hiyo, Spika wa Seneti Amason Kingi aliorodhesha mashtaka hayo kama ukiukaji mkubwa wa Katiba, ukiukaji mkubwa wa Ibara ya Katiba kuhusu uhuru wa Kitaasisi na maamuzi ya majaji, ukiukaji mkubwa wa Katiba kuhusu uaminifu kwa Kiapo na Utiifu kwa mamlaka.
Vile vile, seneti iliidhinisha shtaka la kuamini kwamba Gachagua alitenda uhalifu chini ya Sheria ya Uwiano na Utangamano wa Kitaifa na utovu mkubwa wa nidhamu ambao hauwiani na wito wa juu na hadhi ya Ofisi ya Naibu Rais na Baraza la Mawaziri na Baraza la Usalama la Kitaifa kwa kushambulia hadharani Huduma ya Ujasusi ya Kitaifa (NIS) na Maafisa wake.
Kwa sasa, Prof Kindiki anahudumu kama Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa, jukumu ambalo ameshikilia tangu Oktoba 2022, akapumzishwa kati ya Julai 11, 2024 na Agosti 8, 2024, wakati Rais alipovunja Baraza lake la Mawaziri.
Akiwa Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Taifa, Prof Kindiki ameongoza na kusimamia mageuzi mbalimbali ikiwa ni pamoja na; Mpango wa Uboreshaji wa Vifaa vya Polisi kwa kiasi kikubwa kuimarisha uwezo wa huduma za usalama za Kenya, kukamilika kwa mfumo wa mikakati ya kuanza utekelezaji wa kuboresha Polisi iliyopendekezwa na jopo lililoongozwa na Jaji mstaafu David Maraga na kuimarisha vita dhidi ya ujangili na ukosefu wa usalama kwa ujumla kote nchini, miongoni mwa mafanikio mengine.