Habari za Kitaifa

Kindiki: Mimi huongea kwa ukali lakini siwalengi Wakenya wanaotii sheria ila wahalifu

Na MARY WANGARI August 2nd, 2024 Kusoma ni dakika: 1

PROFESA Kithure Kindiki, amefafanua kuhusu matamshi makali aliyotumia alipokuwa akihudumu kama waziri wa usalama wa ndani.

Bw Kindiki ameshutumiwa kwa kutumia matamshi kama vile “tutawabonda, tutawaangamiza,” yanayodaiwa kuchochea ukatili wa polisi dhidi ya raia hasa katika maeneo yanayokumbwa na ghasia na katika maandamano ya amani.

Bw Kindiki Alhamisi alieleza Kamati Maalum kuwa matamshi yake mazito yalidhamiriwa magaidi, majangili, majambazi na wahalifu wote kwa jumla, na wala sio Wakenya wanaotii sheria.

“Ni kweli nimetumia lugha ya kipekee mno. Watu ninaolenga si Wakenya wanaotii sheria. Huwa ninalenga magaidi, majangili, majambazi, hao ndio ninawaeleza nitawabonda na ninamaanisha hivyo,” alisema Profesa Kindiki.

Akirejelea operesheni ya kuangamiza majangili katika eneo la Bonde la Ufa, Bw Kindiki alisema kuwa, “nilisema nitavunja na kunyoosha miamba na nilifanya hivyo.”

“Nimebomoa na kufurusha majangili na wahalifu waliokuwa wakikimbilia mafichoni kila mara kwenye milima ya Korkor na Nyalecha.”

Kuhusu visa vya polisi kutumia nguvu kupita kiasi, alieleza Kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa, Moses Wetang’ula kuwa polisi wanapaswa kutumia nguvu kwa kiwango kinachoruhusiwa kisheria.

“Wanapokumbana na wahalifu wanapaswa kwanza kuwaamuru wajisalimishe. Wakikaidi na kumtaka kuua polisi, hapo basi sheria inaruhusu wakabiliwe vikali.”