Kindiki: Msiwe na hofu, zile ahadi zote za UDA nitasaidia mimi kuzitekeleza
NAIBU Rais Profesa Kithure Kindiki ameahidi kukweza chama cha United Democratic Alliance (UDA) hadhi zaidi ili kiweze kufikia ndoto yake ya kuleta umoja na maendeleo nchini.
Alisema kinyume na mtangulizi wake Rigathi Gachagua aliyelaumiwa kwa kuendeleza maslahi ya eneo la Mlima Kenya pekee, Profesa Kindiki Jumatatu alisema atahakikisha kuwa maeneo yote ya nchini atayahudumia kwa usawa.
“UDA ni chama cha kitaifa na hivyo kama Naibu Kiongozi wake wajibu wangu utakuwa ni kuendeleza maslahi ya Wakenya wote wala sio eneo fulani au watu wa jamii moja,” akasema.
Profesa Kindiki alisema hayo jana alipopokezwa rasmi wadhifa wa Naibu Kiongozi wa chama hicho kwenye hafla fupi iliyofanyika katika makao makuu ya UDA, jumba la Hustler Centre, jijini Nairobi.
Profesa Kindiki anachukua wadhifa huo ulioshikiliwa na Rigathi Gachagua aliyetimuliwa afisini kama Naibu Rais mwezi jana.
Moja kati ya tuhuma zilizochangia kutimuliwa kwake ilikuwa ni hulka yake ya kutetea maslahi ya eneo la Mlima Kenya na watu wa jamii za eneo hilo.
Kupitia kauli mbinu ya “mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja” Bw Gachagua alishikiza kuwa eneo hilo linapaswa kutengewa kiasi kikubwa cha fedha za maendeleo na huduma nyinginezo kwa msingi wa wingi wa wakazi.
Profesa Kindiki aliwaahidi wanachama kuwa anatawahudumia kwa moyo wake wote ili kuimarisha umaarufu wa chama hicho nchini.
Aidha, aliwapongeza maafisa wake wa chama hicho kwa kuhakikisha kuwa chama kimesalia imara ndani ya wiki kadhaa zilizopita ambapo taifa lilikuwa likipitia mabadiliko yaliyopelekea kuteuliwa kwake kuwa Naibu Rais.
“Mchakato huo wa kikatiba ulihakikisha kuwa afisi ya naibu rais inajazwa ili Wakenya na wanachama wa chama hiki waendelee kupata huduma,” akasema Profesa Kindiki.
Naibu Rais alikariri kuwa ataendelea kuwa mwaminifu kwa UDA huku akiwa tayari kutekeleza majukumu atakayopewa na Rais Ruto.
“Nikuwa sehemu ya safari ambayo chama hiki kimesafiri tangu kilipobuniwa. Wajibu wangu wa kwanza ni kuwa mwanachama mwaminifu wa UDA,” Profesa Kindiki akasema.
“Chama hiki ni kubwa kuliko serikali. Kiongozi wa taifa na serikali kwanza ni kiongozi wa chama kabla ya kuwa rais. Anashikilia afisi ya rais kwa misingi kuwa yeye ni mwanachama wa chama hiki cha UDA,” akaeleza.
Profesa Kindiki alilakiwa katika makao makuu ya UDA na wanachama wa Baraza Kuu la Kitaifa (NEC) wakiongozwa na mwenyekiti Cecily Mbarire na Katibu Mkuu Hassan Omar.