Habari za Kitaifa

Kisa kinachofanana na Mpox chazua wasiwasi Kakamega

Na SHABAN MAKOKHA August 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

MAAFISA wa Afya Kaunti ya Kakamega, wanachunguza kisa kinachofanana na homa ya nyani kilichoripotiwa siku moja baada ya taifa kurekodi kisa cha pili cha virusi hivyo na kuzua hofu kuhusu kusambaa kwa gonjwa hilo nchini.

Mkurugenzi wa huduma za afya nchini, Tabitha Kiverenge, alisema mgonjwa aliyesafiri katika nchi jirani ya Uganda, alionyesha dalili zinazofanana na Mpox.

“Chembechembe kutoka kwa mgonjwa huyo zimepelekwa kufanyiwa vipimo katika maabara ya serikali. Tunasubiri matokeo ili kuthibitisha ikiwa mgonjwa huyo anaugua virusi hivyo au la. Kwa sasa ni tuhuma tu,” alisema Bw Kiverenge.

Mgonjwa huyo alikuwa na homa kali ambayo madaktari walisema ilikuwa zaidi ya vipimo vya kawaida ikiwemo vipele na makovu mwilini.

Kulingana na afisa huyo wa afya, mgonjwa huyo ametengwa na anatibiwa.

Haya yamejiri baada ya Wizara ya Afya kuthibitisha kisa cha pili cha mpox Ijumaa.

Dereva huyo wa trela alifika katika Kituo cha Kufanyia Vipimo cha Port kwenye Mpaka wa Malaba One Stop akiwa na dalili za gonjwa hilo baada ya kusafiri kutoka DR Congo, ambayo ni chimbuko la gonjwa hilo na kupitia Uganda.

Akizungumza katika hafla ya kumkaribisha na Kurejesha Shukran ya Waziri wa Vyama vya Ushirika Wycliffe Oparanya, Waziri wa Afya, Deborah Mulongo alisema mgonjwa huyo aliwekwa karantini katika eneo la Alupe, Busia.

Jumla ya watu 426,438 wamepimwa katika vituo mbalimbali vya kuingia nchini huku chembechembe 43 zikiwasilishwa kwenye labu ili kufanyiwa vipimo vya mpox tangu mlipuko huo ulipozuka.

Kisa cha kwanza cha virusi hivyo nchini kilihusu dereva wa trela wa masafa marefu, 42, kwenye mpaka wa Taita Taveta border na Tanzania kilichoripotiwa Julai 31, 2024.