Habari za Kitaifa

Kitendawili cha kaunti zikiwa na akaunti 1854 benki

Na  WACHIRA MWANGI May 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

KAMATI ya Seneti kuhusu Ugatuzi imesuta kaunti kwa kuendelea kukiuka sheria za usimamizi wa fedha za umma kwa kuwa na akaunti nyingi katika benki za kibiashara.

Katika kikao kilichofanyika katika Hoteli ya Serena Beach, Mombasa, maseneta na taasisi za usimamizi wa fedha walieleza wasiwasi wao kuhusu ukosefu wa uwajibikaji, uwezekano wa matumizi mabaya ya fedha, na udhaifu wa mifumo ya ndani ya udhibiti katika serikali za kaunti.

Kikao hicho, kilichohudhuriwa na maseneta, wawakilishi kutoka Ofisi ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (OAG), Mdhibiti wa Bajeti (CoB), na Baraza la Magavana (CoG), kilibaini kuwa kaunti zilikuwa zikiendesha jumla ya akaunti 1,854, baadhi zikiwa na hadi akaunti 276.

Kaunti za Bungoma, Nyandarua, Kwale, na Kitui zilitajwa kuwa miongoni mwa zilizo na idadi kubwa zaidi ya akaunti za benki.

“Haramu ni haramu. Inawezekanaje kuwe na pesa kwenye akaunti ambazo magavana hawazijui? Kuongezeka kwa akaunti hakuonyeshi uwajibikaji wowote,” alisema Seneta Mteule Margaret Kamar, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Seneta Kamar alisisitiza haja ya mageuzi ya haraka, akihimiza ushirikiano kati ya wadau wa ugatuzi ili kulinda fedha za umma na kuboresha utoaji wa huduma.

“Tuwe na ushirikiano katika juhudi za kutimiza malengo ya ugatuzi. Ni kosa la jinai kuendelea kutumia akaunti zilizorithiwa kutoka kwa manispaa za zamani,” aliongeza.

Mdhibiti wa Bajeti, Dkt Margaret Nyakang’o, alieleza wasiwasi mkubwa kuhusu kutotii sheria zinazodhibiti akaunti za pesa za umma.

“Sijawahi kupokea taarifa yoyote kutoka kwa kaunti kuhusu kufungua akaunti hizo. Baadhi ya kaunti zimeficha akaunti ofisi yangu, na akaunti moja isiyojulikana ilikuwa na Sh1.7 bilioni. Hili ni jambo la kutia hofu,” alisema Dkt Nyakang’o.

Alibainisha kuwa ofisi yake iligundua jumla ya akaunti 110 za ukusanyaji mapato katika benki za kibiashara, kinyume na sheria inayotaka akaunti hizo kuwa katika Benki Kuu ya Kenya (CBK).

Dkt Nyakang’o alitaja Kifungu cha 228 cha Katiba na Kifungu cha 16 cha Sheria ya CoB, ambavyo vinazitaka kaunti kushirikiana kikamilifu na ofisi za usimamizi.

“Kaunti zinaendelea kufungua akaunti bila idhini kutoka Hazina ya Kaunti au Mdhibiti wa Bajeti. Malipo yanayofanyika nje ya mfumo wa IFMIS ni changamoto kubwa kwa ukaguzi,” aliongeza.

Mkaguzi Mkuu wa Hesabu, Nancy Gathungu, alikubaliana na hoja hiyo, akisisitiza kuwa akaunti yoyote yenye fedha za umma lazima ikaguliwe na kufuata sheria.

“Kanuni ya 82 ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma iko wazi: akaunti zote za serikali za kaunti lazima zifunguliwe katika Benki Kuu, isipokuwa kwa malipo ya dharura au pesa ndogo,|”alisema.

Alishangaa ni kwa nini akaunti zilizokiuka sheria tangu mwaka wa 2013 bado hazijafungwa, licha ya kuwepo muda wa miezi sita wa kufuata masharti hayo.

Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya CoG, Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, alitetea uwepo wa akaunti nyingi, akisema baadhi zilifunguliwa kwa masharti ya wafadhili na shughuli zilizorithiwa kutoka kwa manispaa za zamani.

“Tunatambua tatizo hili, lakini tunahitaji mtazamo mpana. Baadhi ya akaunti zilifunguliwa ili kusimamia fedha kutoka kwa washirika wa maendeleo, kama Danida. Nyingine ni za vituo maalum vya afya au elimu,” alisema Gavana Barasa.

Hata hivyo, alitoa wito kwa CoB na OAG kubaini maeneo hatari na akaahidi kushirikiana na Seneti kuhakikisha uwazi.

“Ikiwa kuna visa vya udanganyifu, vitajwe wazi na wahusika wawajibishwe. Hatufai kulaumu wote bali kuchukua hatua kali kwa waliokosea,” alisema.

Lakini Seneta Karungo wa Thangwa wa Kaunti ya Kiambu alikataa hoja hiyo, akiita ukiukaji wa wazi wa sheria.

“Kulingana na OAG, Kaunti ya Kiambu inaendesha akaunti 276. CoB inataja 74. Seneti imefichua 304. Tofauti hii si tu ya kushangaza bali ni jinai,” alisema.

Elgeyo Marakwet, kwa mfano, ilitajwa kuwa na akaunti 129 za vituo vya afya, huku ripoti ya Kaunti ya Nyamira ikieleza kuhusu malipo maradufu kutokana na udhaifu wa usimamizi.

Seneta Mohamed Abbas wa Lamu aliwalaumu magavana kwa uzembe na akaonya kuwa ugatuzi uko hatarini.

“Magavana hawako tena karibu na wananchi. Tatizo si wafadhili, ni ukosefu wa udhibiti wa ndani,” alisema.