Habari za Kitaifa

Kitendawili cha kisanga cha grunedi kwa Wanjigi

Na RICHARD MUNGUTI August 12th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

IDADI ya washukiwa waliokamatwa na kufikishwa kortini kuhusiana na kupatikana kwa grunedi katika makazi ya kiongozi wa chama cha Safina, Jimi Wanjigi imefikia wanne.

Washukiwa wapya, Kennedy Ochieng Asewe na Josiah Augo Otimo walifikishwa mbele ya hakimu mwandamizi Robinson Ondieki mnamo Jumatatu, Agosti 12, 204.

Awali, Dancan Otieno na Calvin Odongo walifikishwa mbele ya hakimu mkuu Bernard Ochoi na kuamuru wazuiliwe siku saba lakini wakili Willis Otieno akaomba uamuzi huo ubatilishwe akisema “Wanjigi amefichua grunedi hizo ni za polisi na wala sio za washukiwa hao wala yeye.”

Mahakimu hao walifahamishwa na Wakili Willis Otieno kwamba “Wanjigi amefichua kwamba grunedi hizo ziliwekwa ndani ya gari lililokuwa limeegeshwa nje ya makazi yake mtaani Muthaiga na polisi usiku wa Agosti 8, 2024.”

Vile vile, Otieno aliwaeleza Mabw Ochoi na Ondieki kwamba “Kaimu Inspekta Jenerali wa Polisi, Gilbert Masengeli aliwaambia wanahabari Agosti 8, 2024 kwamba polisi walipata grunedi hizo ndani ya nyumba ya Wanjigi.”

Alisema Otieno: “Wanjigi amefichua katika kesi aliyowashtaki IG, Mkurugenzi wa Idara ya Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohammed Amin na Mwanasheria Mkuu kwamba polisi ndio waliweka grunedi hizo katika gari lililokuwa limeegeshwa nje ya makazi yake nyumba Nambari 44.”

Wakili huyo aliomba mahakimu wawaachilie huru Otimo, Asewe, Odongo na Otieno akisema “washukiwa hawa ni vibarua wa Wanjigi. Hawajui chochote kuhusu silaha hizi. Wanjigi amedai ni polisi walioziweka ndani ya gari lililoegeshwa nje ya makazi yake.”

Mahakama ilifahamishwa kwamba kuna picha za video zilizonukuliwa na kamera za CCTV zilizo katika makazi ya Wanjigi.

“Ushahidi upo. Wanjigi amedai grunedi ni za polisi. Washukiwa hawa hawajui chochote kuzihusu,” Bw Otieno aliambia mahakama.

Lakini viongozi wa mashtaka James Gachoka, Herbert Sonye na Everlyne Mutisya walipinga ombi la Otieno wakisema polisi wanahitaji muda kukamilisha uchunguzi.

Gachoka alisema grunedi hizo zitapelekewa wataalamu wa silaha kuzikagua kubaini zilikotoka.

Gachoka alisema polisi pia wanataka kutambua walikotoka washukiwa hao kwa vile hawakuwa na vitambulisho.

Awali, Otieno alisema polisi wamekaa na washukiwa hao kwa siku tano na wangekuwa wamekamilisha uchunguzi wao.

Alisema Asewe na Otimo walitiwa nguvuni mtaani Soweto Dandora na wala hawakutiwa nguvuni na polisi katika makazi ya Wanjigi.