Kitendawili cha mwanamume kutoweka kiajabu akikwea Mlima Kenya
FAMILIA moja kutoka Nanyuki, Kaunti ya Laikipia, inaomba serikali iingilie kati katika juhudi za kumtafuta ndugu yao aliyetoweka katika Mlima Kenya siku 14 zilizopita alipokuwa kwenye shughuli ya kupanda mlima huo.
Bw Samuel Macharia, 35, na mwelekezi wa wanaokwea mlima, alitoweka Desemba 23, 2025. Alikuwa ameandamana na waelekezaji wengine wanne waliokuwa wakiwasindikiza watalii wawili kutoka Japan katika safari ya kupanda Mlima Kenya.
Kwa mujibu wa kaka yake mkubwa, Daniel Kagwaini, ambaye alikuwa sehemu ya kundi hilo, waliondoka mjini Nanyuki asubuhi kupitia njia ya Sirimon na kufika katika kambi ya Shiptons majira ya saa nane mchana baada ya matembezi magumu ya takribani saa saba.
Ni katika kambi hiyo walipogundua kuwa Bw Macharia, ambaye alikuwa amepewa jukumu la kubeba vyakula, alikuwa ametoweka.
Bw Kagwaini anasema ndugu yake ni mwongozaji wa wapanda mlima mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 15 ya kuongoza wageni na kuzunguka maeneo hatari ya Mlima Kenya.
Aliongeza kuwa hata siku hiyo, hakukuwa na dalili zozote za ugonjwa au mwenendo wa ajabu kutoka kwake.
“Nimefanya kazi na ndugu yangu kwa miaka mingi na hatuwezi kueleza kilichotokea. Alipotea nikiwa naye. Nilirejea tulikopita lakini sikupata chochote. Nimemtafuta zaidi ya mara tatu bila mafanikio,” alisema Kagwaini.
Wakati huohuo, alisema kinachochanganya familia na marafiki ni kwamba wakati wa kumtafuta, walipata baadhi ya vitu vya kibinafsi vinavyoaminika kuwa vya Macharia, vikiwemo kitambulisho cha kitaifa na simu ya mkononi, pamoja na vyakula alivyokuwa amebeba, vikiwa vimepangwa kwa utaratibu kando ya njia ya watembea kwa miguu.
Alibainisha kuwa tukio hilo liliripotiwa katika vituo vya polisi vya Chogoria na Timau kwa matumaini kuwa ndugu yao mdogo atapatikana akiwa hai.
Mnamo Jumanne, Januari 5, tulimkuta shangazi yake Lucy Kagwaini pamoja na wanafamilia wengine wakiwa wamekaa kwa huzuni kando ya barabarani katika Kambi ya Old Moses.
Walikuwa wakitazama vilele vya mlima wakisubiri majibu, wakitumaini muujiza au angalau kikomo cha fumbo hili la kutatanisha.
“Yuko mahali fulani; sijui kama ni msituni au mlimani hapa. Tumejitahidi kadri tuwezavyo lakini hatujamuona. Tunaomba serikali itusaidie. Huyu ni mpwa wangu na hatuna njia nyingine,” alisema Bi Lucy Kagwaini huku akijaribu kuzuia machozi.
Familia hiyo ina matumaini kuwa ndugu yao huenda alichanganyikiwa akaingia kwenye misitu mikubwa ya Mlima Kenya na atapatikana akiwa hai katika vijiji jirani.
Wanaamini huenda alipata maradhi ya Altitude Cerebral Edema (HACE), hali inayosababisha kuchanganyikiwa sana na kuona vitu visivyokuwapo kwa wanaokwea mlima.
Shirika la Huduma ya Wanyamapori Kenya (KWS) limeanza kumtafuta mkwea huyowa mlima.
Mlima Kenya umewahi kushuhudia matukio ya wapandaji kupotea na hata kupoteza maisha. Hata hivyo, kisa cha Macharia, ambaye alikuwa na tajriba ya zaidi ya muongo mmoja ya kuzunguka maeneo magumu ya mlima huo, kimewaacha marafiki na familia yake katika mshangao na huzuni kubwa.