Habari za Kitaifa

KNUT yaondoa notisi ya mgomo, yaelekeza walimu waingie kazini Jumatatu

Na LABAAN SHABAAN August 25th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

CHAMA cha Walimu nchini (KNUT) kimeambia walimu wafike kazini kwa masomo ya muhula wa tatu baada ya kuondoa notisi ya mgomo.

Walimu walikuwa tayari kubwaga vifaa vya kazi kuanzia Jumatatu Agosti 26, 2024 baada ya vyama vya walimu kutoa notisi ya mgomo wa kitaifa uliowaelekeza walimu wakae nyumbani hadi matakwa yao yote yashughulikiwe na serikali.

Kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, Katibu Mkuu Collins Oyuu ametangaza kuwa malalamishi ya walimu yanashughulikiwa kiutawala.

Haya yakijiri, Chama cha walimu wa shule za upili na vyuo (KUPPET) kimetangaza mgomo wa walimu kuanzia Jumatatu kama ilivyopangwa awali. Wanachama 68 wa Baraza la Kitaifa KUPPET waliunga mkono mgomo huo dhidi ya wawili.