Habari za Kitaifa

Korti yakataa kuagiza polisi kuachilia vijana waliotekwa nyara

Na RICHARD MUNGUTI April 11th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MAHAKAMA Kuu, Alhamisi, Aprili 10, 2025 ilikataa kuamuru polisi kuwaachilia vijana wawili waliotekwa nyara Desemba 2024.

Uamuzi huu ni afueni kwa Inspekta Jenerali Douglas Kanja na Mkurugenzi wa Uchunguzi wa jinai (DCI) Mohamed Amin ambao korti ilikuwa imeombwa iwaagize kuwafikisha kortini Stephen Mbisi Kavingo na Kevin Muthoni.

Akitupilia mbali ombi la kuachiliwa kwa Stephen Mbisi Kavingo na Kelvin Muthoni, Jaji Bahati Mwamuye alisema hakuna ushahidi uliowasilishwa kuthibitisha wahasiriwa hao wako mikononi mwa polisi.

Jaji Mwamuye alisema kwamba walalamishi katika kesi hiyo – Chama Cha Mawakili Kenya (LSK), Kituo Cha Sheria na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Binadamu (KNHRC) – hawakuwasilisha ushahidi kuthibitisha kabisa wahasiriwa wanazuiliwa katika korokoro za polisi.

Kavingo na Muthoni walikamatwa na watu wanaoaminika kuwa maafisa wa polisi Desemba 2024.

“Masuala mazito kisheria ambayo walalamishi (LSK, Kituo na KNHRC) wamezua yanaweza tu kutathminiwa baada ya kesi hizi kusikizwa na ushahidi kuwasilishwa,” alisema Jaji Mwamuye.

Jaji huyo alikataa kushurutisha Inspekta Jenerali wa Polisi David Kanja Mkurugenzi wa Uchunguzi wa Jinai (DCI) Mohamed Amin na Waziri wa Masuala ya Usalama Kipchumba Murkomen kuwaachilia wahasiriwa hao.

Jaji huyo aliamuru kesi hiyo itengewe siku ya kusikizwa baada ya Likizo ya Pasaka iliyoanza Aprili 9 na itakamilika Aprili 23, 2025.

Kupitia kwa rais wa LSK, Faith Odhiambo, familia za Kavingo na Muthoni zilieleza masikitiko makubwa kwa vile Serikali ilinyamaza kimya na haikusema chochote kuhusu kutekwa nyara kwa wapendwa wao na watu wanaodhaniwa kuwa maafisa wa polisi.

Mahakama iliombwa iamuru polisi wawafikishe kortini wahasiriwa hao na kuwafungulia mashtaka ikiwa wamevunja sheria.

Jaji Mwamuye aliombwa na walalamishi atetee haki za wahasiriwa kwa kuamuru kuachiliwa kwa Kavingo na Kevin.

Mahakama ilielezwa wahasiriwa hao walikamatwa na kuwekwa ndani ya magari yenye nambari za usajili za raia.