Maafisa wa serikali watahitaji leseni kushiriki harambee
MAAFISA wakuu wa serikali na watumishi wa umma hivi karibuni watahitajika kupata leseni ili kushiriki harambee ikiwa mswada wa kudhibiti shughuli hiyo utapitishwa.
Mswada wa Kuitisha Michango kutoka kwa Umma wa 2024 uliodhaminiwa na Seneta wa Kericho Aaron Cheruiyot unalenga kuweka mwongozo wa kisheria kusimamia uendeshaji wa michango na kuendeleza uwazi na uwajibikaji katika uendeshwaji wa shughuli hiyo.
Mswada huo pia unalenga kuwakinga Wakenya wasipunjwe kupitia michango feki ya harambee huku ukiweka mwongozo wa kutoa hamasisho kwa umma ili wafanye maamuzi ya busara wanaposhiriki harambee.
Mswada huo pia unapendekeza adhabu kali kwa wale watakaovunja sheria kuhusu harambee.
“Afisa Mkuu wa serikali au mtumishi wa umma atakayepatikana na hatia ya kuvunja hitaji la kifungu hiki atatozwa faini isiyozidi Sh5 milioni,” inasema kifungu cha 13 cha mswada huo.
Kosa hilo linafananishwa na kosa la uchaguzi ambapo anayepatikana na hatia huzimwa kuwania.
Wanasiasa wanaopania kuwania nyadhifa za umma pia wanazuiwa kushiriki harambee, miaka mitatu kabla ya uchaguzi mkuu.
Sheria hiyo pia inamlazimu aliyefaidi kutokana na michango ya harambee kutaja kiini cha michango hiyo na kuwasilisha maelezo hayo ya Mamlaka ya Ukusanyaji wa Ushuru Nchini (KRA).
“Mtu atakayetoa michango ya harambee au yule atakayepokea fedha hizo sharti atoe maelezo kwa KRA kwa mujibu wa Sheria ya Ushuru,” mswada huo mpya unasema.
Raia wa kawaida watakaopatikana na hatia ya kukiuka sheria hii watatozwa faini isiyozidi Sh2 milioni au watupwe gerezani kwa miaka mitatu.
Mswada huo unajiri wakati ambapo vijana wa Gen Z wamelalamika kuwa baadhi ya wanasiasa wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza wamekuwa wakitoa pesa nyingi kupita kiasi katika michango ya harambee ilhali raia wa kawaida wanazongwa na ugumu wa miasha.
“Mswada huu umetayarishwa kwa lengo la kuhakikisha kuwa Harambee inatumika kama majukwaa ya kuwasaidia Wakenya wala sio kuendeleza ufisadi, ubadhirifu wa pesa za umma na maovu mengine ya kiuchumi. Kulingana na Seneta Cheruiyot, ambaye ni kiongozi wa wengi katika Seneti, mswada huo pia unalenga kupunguza tabia ya kutegemea michango ya harambee iliyokithiri katika jamii.
Harambee pia zimetumika kusaka fedha kwa kugharamia matumizi ya kibinafsi.
“Mswada huu unalenga kuhakikisha kuwa harambee haitumiwi kushughulikia masuala ya kibinafsi,” anasema Bw Cheruiyot.
Seneta huyo wa Kericho anaeleza kuwa serikali inafaa kutoa vishawishi kwa watu ambao wako tayari kutoa michango kwa hiari yao.
Sheria iliyoko sasa ya kusimamia michango ya harambee ni dhaifu na haitoi vishawishi kwa wanaotoa michango hiyo na inawaacha nje watu ambao sio maafisa wa serikali.
Mbunge wa Kapsaret Oscar Sudi amewahi kushutumiwa kwa kutoa Sh20 milioni, wakati mmoja, katika harambee.
Shutuma hizo haswa kutoka kwa vijana wa Gen Z zilimlazimisha Rais William Ruto kutoa amri ya kuzima maafisa wa umma kushiriki harambee.
Aidha, Dkt Ruto aliagiza Afisi ya Mwanasheria Mkuu kuandaa sheria ya kudhibiti harambee na hivyo kushughulikia malalamishi ya Gen Z.