Maelfu kupoteza marupurupu ya kuhudumu katika mazingira magumu
MAELFU ya Watumishi wa Umma wanaonufaika kwa sasa na marupurupu ya kuhudumu katika mazingira magumu wanatarajiwa kukosa malipo hayo serikali ikitekeleza ripoti iliyochunguza upya maeneo yanayoainishwa kuwa yenye mazingira magumu.
Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi, alieleza Bunge la Kitaifa kwamba kuorodhesha upya maeneo yenye mazingira magumu kutawezesha serikali kupunguza malipo ya marupurupu kutoka Sh25.98 bilioni hadi Sh19.53 bilioni.
“Ningependa kufahamisha Bunge kwamba utekelezaji wa ripoti ya Kamati ya Kiufundi ya Mashirika Mbalimbali utapunguza gharama za kifedha za malipo ya marupurupu ya mazingira magumu kutoka Sh25 bilioni hadi Sh19 bilioni kwa mwaka na hivyo kuiwezesha serikali kuokoa Sh6 bilioni. Hii ni kutokana na pendekezo la kuanisha maeneo ya mazingira magumu katika utumishi wa umma,” alisema Bw Mudavadi.
Bw Mudavadi alikuwa akirejelea ripoti ya kamati ya kiufundi iliyojumuisha wadau mbalimbali kuhusu sera zinazotumika katika kuainisha maeneo ya mazingira magumu pamoja na malipo ya marupurupu hayo katika utumishi wa umma.
Hata hivyo, licha ya ripoti hiyo kukamilika mwaka wa 2019, haijawahi kutekelezwa.
Bw Mudavadi aliwaambia wabunge kwamba serikali sasa imeazimia kutekeleza ripoti hiyo na kuongeza kuwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yameainishwa kama yenye mazingira magumu yataondolewa kulingana na mapendekezo ya kamati.
Alisema matokeo ya ripoti hiyo yaliwasilishwa kwa Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC), ambayo itatangaza viwango vipya mara tu maeneo hayo yatakapochapishwa kwenye gazeti rasmi la serikali.
Bw Mudavadi alisema maeneo yatakayoorodheshwa kuwa yenye mazingira magumu pia yamewasilishwa kwa Mkuu wa Watumishi wa Umma kuchapishwa rasmi.
Alieleza Bunge kuwa moja ya matokeo muhimu ya kamati hiyo ya kiufundi ni kwamba baadhi ya maeneo yaliyotajwa awali kuwa yenye mazingira magumu, hayakuhitimu kuwa hivyo.
Kamati hiyo pia ilibaini kuwa kwa sasa baadhi ya maeneo yaliyotangazwa kuwa yenye mazingira magumu yanahusisha kaunti nzima, tarafa au sehemu ya kanda. Hata hivyo, baada ya uchambuzi, ilibainika kuwa ni maeneo maalum tu ndani ya maeneo hayo yanayostahili kuainishwa hivyo.
Maeneo hayo, kulingana na Bw. Mudavadi, yameondolewa na kuorodheshwa ipasavyo.
Zaidi ya hayo, ripoti ya kamati hiyo ilibaini kuwa si watumishi wote wa umma walio maeneo yenye mazingira magumu wanaopokea marupurupu kutokana na tofauti katika mwongozo wa sera za utumishi wa umma.
Kamati hiyo pia ilibaini kuwa baadhi ya maeneo yaliyokuwa yakitajwa kama yenye mazingira magumu yamebadilika kufuatia kuanzishwa kwa mfumo wa ugatuzi ambao umechochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi kote nchini.
Bw Mudavadi alisema tofauti katika uainishaji wa maeneo yenye mazingira magumu zimesababishwa na ukosefu wa sera ya pamoja, ambapo mashirika mbalimbali ya serikali huainisha maeneo kwa kutumia viwango tofauti.
“Imebainika kuwa viwango vinavyotumika kutathmini maeneo yenye mazingira magumu havijaunganishwa. Kwa mfano, Utumishi wa Umma hutumia mipaka ya zilizokuwa wilaya, ilhali Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) hutumia maeneo ya elimu,” alisema Bw Mudavadi.
Kwa sasa, Utumishi wa Umma, serikali za kaunti na mashirika ya umma yanatambua maeneo 16 kuwa yenye mazingira magumu; sekta ya elimu ina maeneo 44, huku Idara ya Mahakama ikiwa na maeneo 21.