Magavana sita wasafiri ng’ambo ‘kutafuta pesa za maendeleo’
MAGAVANA sita wa Pwani wamesafiri Italia kusaka fedha za miradi ya maendeleo katika sekta ya Uchumi wa Baharini.
Kupitia muungano wao wa Jumuiya ya Kaunti za Pwani (JKP), magavana hao, wakiongozwa na mwenyekiti wao Bw Gideon Mung’aro (Kilifi), Abdulswamad Nassir (Mombasa), Fatuma Achani (Kwale)Dado Godhana (Tana River), Issa Timamy (Lamu), na Andrew Mwadime (Taita Taveta), wanasaka fedha za kuimarisha sekta ya uchumi wa baharini ili kufufua uchumi na nafasi za ajira kwa vijana.
Bw Mung’aro alisema magavana hao wa Pwani waliamua kusafiri hadi Italia kusaka wawekezaji wa sekta hiyo ili kuimarisha uchumi wa baharini.Alisema wanalenga kununua mashua kubwa ambazo zitawasaidia wavuvi kuvua samaki katika bahari kuu.
“Hii ni safari ya magavana kupitia muungano wetu wa JKP, magavana wote na idara zetu zote za uchumi wa baharini katika kila kaunti na hata wawakilishi kutoka serikali ya kitaifa. Tunaenda kujadili maswala ya kukuza uchumi wetu kupitia sekta ya uchumi wa baharini,” alisema Bw Mung’aro.
Bw Mung’aro alisema magavana hao pia watafanya mkutano na Waziri anayehusika na masuala ya Kigeni na Biashara.
“Ni mkutano ambao tunaenda kusaka ufadhili wa uchumi wa baharini hasa wavuvi. Unaona Kilifi tayari nimeanzisha boti 43. Ninataka kuendeleza sekta hii, awamu ya pili tunalenga kupeana boti kubwa ambazo zinaweza kwenda katika maji makuu,” aliongeza Bw Mung’aro.
Baadaye, Bw Mung’aro atakutana na viongozi wakuu wa serikali ya Italia. Gavana huyo ambaye ana uhusiano wa karibu na Waitaliano kupitia marafiki zake akiwemo bwanyenye mashuhuri Bw Flavio Briatore, alisema atatumia fursa hiyo kusaka wawekezaji.
Alisema kuwa alipokuwa meya wa Malindi zaidi ya miaka 15 iliyopita, aliunda uhusiano wa karibu na Waitaliano. Aliwarai kina mama kutoka eneo la Pwani kujitosa kwenye sekta ya uchumi samawati hasa uvuvi.
“Nina bahati kwa sababu nitakuwa na mikutano na baadhi ya mawaziri wa Italia kuhusu swala la kufufua utalii. Unajua binafsi waziri mpya wa Utalii huko Italia ni rafiki yangu mkubwa, tumekuwa naye miaka mingi tunajuana akiwa Malindi, ni rafiki ya rafiki zangu kama Bw Briatore. Naibu Waziri wa Fedha pia ni rafiki yangu,” alisema Bw Mung’aro.
Bw Briatore anamiliki hoteli kubwa mji wa kitalii wa Malindi ambao kwa muda umekuwa ukimilikiwa na raia wa Italia Hata hivyo, wakati wa janga la Covid-19 mwaka wa 2020, Waitaliano wengi walihepa Malindi na kurudi makwao.
Bw Mung’aro alisema atawaregesha raia hao ambao walikuwa wamewekeza katika mji huo na wengine wapya ili kufufua sekta ya utalii wa kimataifa.
“Tulikutana na Balozi wa Kenya nchini Italia, Bw Fredrick Matwang’a, kujadili maswala ya kukuza sekta ya uchumi samawati,” aliongeza.
Gavana huyo alisema pia atajadili swala la upanuzi wa uwanja wa ndege wa kimataifa wa Malindi. “Waitaliano wameapa kushirikiana nasi kwenye upanuzi wa kiwanja hicho cha ndege ili kukuza sekta ya utalii. Ndio maana nimetilia mkazo umuhimu wa umoja wa Wapwani,” aliongeza.